14 October, 2015

Magufuli azungumzia samaki, Lowassa ageukia madini


Magufuli azungumzia samaki.

Mgombea wa urais kupitia Chama Cha mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akiwa rais ataendelea kukamata meli za kigeni zinazovua samaki kwenye bahari ya Tanzania kinyume cha sheria kama alivyowahi kufanya akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Alisema hatakubali kuona samaki wa Tanzania wanageuzwa shamba la bibi, hivyo samaki watakaokamatwa kwenye meli zinazovua kiholela watagawiwa kwa wananchi kama kitoweo. Dk. Magufuli alisema hayo kwenye mikutano yake ya kampeni katika majimbo ya Mchinga na Kilwa Kusini mkoani Lindi na pia Kibiti mkoani Pwani.

Mgombea huyo alisema kuna watu wanamchonganisha na wavuvi kwa kudai kwamba akiingia madarakani atachoma nyavu zao na hawatakuwa na fursa za kuendesha shughuli zao.

Alisema yeye atakuwa rafiki mkubwa wa wavuvi wadogo na atawawezesha kwa mikopo na zana bora za uvuvi ili wavue kisasa na kuondokana na umaskini. Alisema atapambana na meli kubwa za uvuvi ambazo zimekuwa zikiiba samaki ambao ni mali ya Watanzania.

Sitaruhusu samaki walio kwenye bahari yetu wawe shamba la bibi. Wanaojijua kuwa wanaiba samaki wetu arobaini zao zimefika, mimi nitakamata na kugawa bure kwa wananchi, maana samaki ni mali yao…. kama niliweza kufanya hivyo nikiwa waziri wa kitoweo, siwezi kushindwa nikiwa rais,” alisema.

Lowassa ageukia madini

Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 atahakikisha mikataba yote mibovu ya madini inapitiwa upya ili kujenga uchumi imara kwa manufaa ya taifa.
 
Lowassa ambaye alishaahidi kuifumua pia mikataba ya mafuta na gesi wakati akiwa mkoani Mtwara, aliyasema hayo jana kwenye mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni katika kata ya Katoro, Jimbo la Busanda mkoani Geita.
Iwapo nitashinda na kuwa rais, nitahakikisha mikataba mibovu ya madini na gesi inapitiwa tena ili kulinufaisha taifa,” alisema na kushangiliwa na maelfu ya watu waliojitokeza kwenye mkutano huo.
 
Mgombea huyo anayeungwa mkono pia na vyama vingine vinavyounda muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema mbali na kupitia mikataba ya madini na gesi, pia atahakikisha kuwa anaibadili Tanzania na kulikabili kwa ukamilifu tatizo la umaskini linalowakabili mamilioni ya wananchi. 
 
Kadhalika, alisema serikali atakayoiongoza itaboresha elimu na kilimo, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakwamua Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini.
-Nipashe

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...