15 August, 2015

Zijue Sifa 10 za mgombea urais bora wa upinzani 2015

Lengo la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania waanze kuwafahamu viongozi wao wajao na hata aina ya sifa wanazoweza kuwa nazo. Inawezekana kabisa kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee mmoja wao kugombea au la, lakini hapa ninachoangalia ni kwamba tayari wananchi watakuwa “wamesogezwa karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata akiletwa mgombea kutoka wapi, walau wananchi watakuwa wanajua wafanye uamuzi wa namna gani.

Ni jana tu nimemaliza uchambuzi wa watu wanaotajwa au waliojitokeza kugombea urais au wale ambao hawajajitangaza na hawana nia lakini jamii ndani na nje ya vyama vyao inawataja kama watu wenye sifa, uwezo na hata vigezo vya kuiongoza nchi yetu, kutoka vyama vya upinzani.

Lengo la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania waanze kuwafahamu viongozi wao wajao na hata aina ya sifa wanazoweza kuwa nazo. Inawezekana kabisa kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee mmoja wao kugombea au la, lakini hapa ninachoangalia ni kwamba tayari wananchi watakuwa “wamesogezwa karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata akiletwa mgombea kutoka wapi, walau wananchi watakuwa wanajua wafanye uamuzi wa namna gani.

Leo nahitimisha hoja ya wagombea wa upinzani kwa kutoa sifa 10 za mgombea urais bora kutoka upinzani ambaye anaweza kupigiwa kura nyingi na Watanzania na hatimaye kuwa rais mpya wa Tanzania:

1. Mwenye umaarufu/umashuhuri na anayekubalika

Sifa hii ni muhimu, unapokuwa nje ya dola na nje ya chama tawala siyo rahisi kukishinda chama kinachoongoza Serikali. Umaarufu, umashuhuri na kukubalika ni mambo ya lazima. Ukitizama historia ya dunia na hata Afrika, vyama vikongwe vilipoondolewa madarakani waliofanya hivyo walikuwa wapinzani mashuhuri. Umuhimu wa sifa hii ni kuwa walau mtu maarufu na mashuhuri au anayekubalika, tayari amewekeza “mbegu” kwenye mioyo ya wananchi, wanaweza kumwamini ili waondoe hatima ya nchi mikononi mwa chama kilichowaongoza kwa miaka 50 na kuiweka mikononi mwa watu wapya. Wananchi wasipomwamini kiongozi wa upinzani anayekuja kwa sababu wanamkubali, ndipo huzuka ile kasumba ya “tupige kura kwenye zimwi likujualo”.

Hatari ya sifa hii

Umaarufu, umashuhuri na kukubalika vitaweza kufanya kazi kwa upinzani ikiwa mgombea husika hatatumia mwanya wa kukubalika kwake kujenga kiburi na hatimaye kuwasaliti wananchi. Ndiyo kusema kuwa vyama vya upinzani vitapaswa kuchagua mtu bora ambaye atatimiza matakwa ya wananchi “hata kama ni maarufu kuliko jua”.

2. Atakayebeba ajenda bora na kuifafanua vizuri

Kubeba ajenda bora na kuwa na uwezo wa kuifafanua kwa lugha rahisi ni jambo la muhimu kwa mtarajiwa kutoka upinzani. Moja kati ya makosa makubwa ya vyama vya upinzani katika bara la Afrika ni kutaka kubeba ajenda nyingi na kumrundikia mgombea urais, nakubali kuwa Afrika ina matatizo katika kila sekta ya maisha ya mwanadamu, lakini lazima iwe na vipaumbele vinavyowaumiza wananchi. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na ajenda bora kuliko ile ya CCM na atapaswa kuwa na uwezo wa kuifafanua akaeleweka na mipango ya utekelezaji wake ikawa siyo ya “kusadikika”.

Hatari ya sifa hii

Ni pale inapotokea kuwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani anazunguka nchi na ajenda iliyo bora kabisa lakini utekelezaji wake ukifanana au kushabihiana moja kwa moja na ule wa mgombea wa CCM. Wananchi wakiona upinzani unahubiri mipango na mbinu zilezile za CCM wataamua pia kuchagua “shetani wanayemjua” ili kujiweka kwenye mazingira ya usalama zaidi. Hivyo, ajenda ya mgombea bora wa upinzani na utekelezaji wake vinapaswa kuwa “vya kipekee”.

3. Mwenye uzoefu na rekodi ya uchapakazi

Uzoefu wa uongozi na uchapakazi unaofahamika ni jambo la msingi kwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani. Vyama vya upinzani haviwezi kushinda uchaguzi na mgombea bora vitakayekuwa naye ikiwa mtu huyo si mzoefu na mchapakazi anayefahamika, mtu mwenye kujali wengine katika kazi lakini ambaye wananchi wataamini kuwa huyu atasimama pamoja na sisi usiku na mchana kuleta mabadiliko ya nchi.

Katika siasa, wananchi hupaswa kwanza kuamini na kisha hufanya uamuzi. Ikiwa mgombea bora wa urais wa upinzani hatakuwa na rekodi za uzoefu wa utumishi (katika taasisi za dini, serikali, vyama vya siasa na nyinginezo) si rahisi kumuuza kwa wananchi. Pia, ni lazima awe ni mtu ambaye rekodi zake zinatajwa kuwahi kuleta mabadiliko makubwa mahali alipofanya kazi.

Hatari ya sifa hii

Sifa hii hupaswa kuelezewa na kufahamika kwa wananchi kutoka kwa timu za kampeni za wagombea, wakati mwingine wapambe wa wagombea huchukua muda mwingi kutaja elimu ya mgombea wakidhani wananchi wanachagua elimu, kumbe elimu ni jambo moja tu kati ya sifa 100 za kiongozi. Ikiwa sifa hii muhimu haielezwi kwa uwazi kwa wananchi na hasa kwa kutaja rekodi bora za mgombea wa upinzani, wananchi wanaweza kumpa kisogo.

4. Mwenye uadilifu usio na shaka

Mgombea bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa kuwa na uadilifu uliotukuka, usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana kuwa, awe ni mtu ambaye uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa Taifa zima. Awe na rekodi za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina maana kuwa, wananchi wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka haraka wasimame na kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”. Marais wengi walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na Marekani kwa kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa hii.

Hatari ya sifa hii

Kigezo hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo uelewa wa wananchi vijijini na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu nao huweza kuchafuliwa ndani ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si ajabu mgombea akawa hata na uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili kimchafue mwenzake, sifa za mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope. Vyama vya upinzani vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha uadilifu wa mgombea wake unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na propaganda za CCM.

5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua uchumi

Moja ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania ni usimamizi wa uchumi. Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa kutekeleza mipango yetu kwa sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila dakika na ambao hauna dira. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu ambaye akisimama na kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote wanamwelewa, kwamba “naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa umaskini wa nchi”.

Hatari ya sifa hii

Ni pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango kabambe ya uchumi lakini yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa umaskini, lakini pia ni pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi. Katika nchi maskini, wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi ili kuwahakikishia wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza kutekelezeka kwa wakati

6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa

Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa mtu wa kipekee ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano dhidi ya rushwa, ndogo na kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba anapiga vita rushwa, bali anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu ambaye yuko mbali kabisa na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani watatafuta mgombea wa namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule wa CCM, kwamba ukiwaweka pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme “…naam huyu wa upinzani anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”

Hatari ya sifa hii

Ikiwa upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika mapambano ya rushwa lakini ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya mipango ya upinzani inapaswa kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya ya usimamizi wa mapambano dhidi ya rushwa na hata kueleza watu watakaokuwa na sifa za kufanya kazi na mifumo hiyo.

7. Asiyependa kulipiza visasi na atakayefuata sheria

Jambo hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka upinzani anapaswa kuwa na sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa kutokuwa na tabia ya kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa ya sheria katika utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya kisheria ambayo ni lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate, mfano, wizi wa pesa za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi upo, lazima watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala kupotea”. Lakini kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo yalikuwa yanatendwa na uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na zisizo na maana, hayana haja ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.

Hatari ya sifa hii

Wananchi wengi huhofia masuala ya usalama iwapo vyama vipya vitaingia madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo hupoteza usalama ni “kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani vinawajibika kuwa na mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya nyuma ya kiutendaji, ila atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa makusudi na kwa kutofuata sheria.

8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi

Tangu tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika kwa kuwa na mifumo mibovu na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni janga kubwa. Rais bora ajaye kutoka upinzani ana kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi katika kila eneo ili mifumo ifanye kazi kwa mbio na kwa tija kubwa zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka ya 1990 na bado wako gerezani bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari Kilombero na huko bei ya sukari ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni matatizo makubwa ya kimfumo. Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuja kubadilisha kabisa mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa bahati nzuri, upinzani unaweza kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo havikuwahi kuongoza Serikali na vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.

Hatari ya sifa hii

Ubadilishaji wa mifumo ukifanywa haraka na kwa pupa, utaingilia na kuvunja hata mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na kukomaa kwa upande chanya. Ni jukumu la mgombea bora wa upinzani na timu zake kutambua mifumo yote ya utendaji katika sekta za jamii na kubainisha tangu wakati wa kampeni, ipi itavunjwa na ipi itarekebishwa ili kutoleta hofu yoyote kwa wapiga kura.

9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba

Suala la katiba mpya ni ajenda muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe kuwa na busara za kutosha na msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba na hasa mchakato wa Katiba Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na misimamo ya wananchi katika suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama katiba itapitishwa au la na hatuelewi kama wananchi wanaikubali au wanaikataa. Nani atatuvusha na kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo mgombea bora wa urais kutoka upinzani.

Hatari za sifa hii

Msimamo wowote ule wa mgombea urais wa upinzani katika jambo hili unaweza kuwa na athari chanya au hasi kulingana na namna wananchi wanavyolitazama suala la katiba. Kama mgombea huyu atakuwa na msimamo katika kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi, jambo hili peke yake litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa kinyume chake, litakuwa na athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama athari yenyewe ni chanya au hasi.

10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa

Moja ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni kuliwakilisha Taifa katika masuala ya kimataifa. Rais bora kutoka upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya masuala ya kimataifa, si kuishi Ulaya na Marekani, lakini kuwe na ushahidi wa kutosha kuwa amewahi kushiriki katika baadhi ya shughuli muhimu za kimataifa na kwamba huenda hata kimataifa yeye ni mtu bora. Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea mwenye sifa hii pia, ni jukumu la upinzani pia kuwa na mtu ambaye amejipanga vyema kimataifa na mambo aliyoyasimamia kimataifa pia yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali, yanaweza kuwa ya kijamii, ya kitaasisi au ya kitaaluma.

Hatari ya sifa hii

Sifa hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za kuisaidia CCM, kwamba ndicho chama pekee chenye watu waliofanya kazi za kimataifa na wataifanya Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea ambaye tayari wananchi wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na shaka ili kusiwe na tabu ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura juu ya eneo hili.

HITIMISHO

Andiko hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote muhimu za kiongozi bora kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha Taifa. Nimechokoza mjadala wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya kuongoza Serikali si nyepesi, inataka kujipanga kila idara na kuwathibitishia wapigakura kuwa mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura huwa ni kutafuta namna gani watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati nzuri vyama vya upinzani katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya kupigiwa mfano inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji na utendaji kazi bora.

-Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...