Akizungumza jana kwenye kongamano la Diaspora, Membe ambaye alivuka hatua ya awali ya mchujo akiwa mmoja wa watu watano ambao majina yao yalipelekwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, alishika nafasi ya mwisho kwenye kura akiwa nyuma ya Dk John Magufuli, Balozi Amina Salum Ali, Dk Asha-Rose Migiro na January Makamba.
Tangu ashindwe kwenye kura hizo mapema mwezi uliopita, waziri huyo hakuwahi kuzungumzia kuanguka kwake, lakini jana aliweka bayana hisia zake.
“Kwenye mpira unaweza kupata timu nzuri sana inacheza kwenye ligi, ikafanya vizuri,” alisema.
“Lakini mwishoni inapotoka droo (sare) na timu nyingine, timu zinakwenda kwenye penalti. Sasa inaweza kutokea ikafungwa penalti zote tano na timu nyingine ambayo wewe hukutegemea ikashinda vizuri tu.
“Kwenye lugha ya kimichezo, kile kitendo cha timu iliyocheza vizuri ikashindwa kwenye penalti, maana yake inakufa kifo kinachojulikana kama sudden death (kifo cha ghafla). Inapopata sudden death, huitegemei isimame na kueleza kilichotokea.”
Membe alikuwa anaonekana kuwa mmoja wa makada waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye urais, lakini alianguka vibaya kwenye kura za wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Kuhusu kongamano hilo la siku tatu alilofungua kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema licha ya kuwa anakaribia kuondoka madarakani atahakikisha anaendelea kupambana ili Watanzania wanaoishi nje wapate uraia wa nchi mbili.
“Ndipo tutakapopata maendeleo ya kweli ya wanadiaspora. Wanadiaspora watakuwa na kazi nzuri watakapokuwa nchi za nje na watakuwa wanaingiza mabilioni ya fedha nchini kama ilivyo kwa Kenya na Nigeria,” alisema.
Alisema hivi sasa Watanzania hao wanashindwa kusafirisha fedha zao kwa wingi nchini kwa sababu wengi wao ‘wamejilipua’ kwa hiyo wanazituma kinyemela, lakini pale watakapopata fedha wakiwa na uraia wa nchi mbili, wataweza kutuma bila kuficha.
“Natoka huku nikiendelea kuamini kwamba diaspora ya kweli ya Tanzania na isiyo na woga wowote ni pale watakapopata pesa za kufurahia uraia wa nchi mbili,” alisema.
No comments:
Post a Comment