Mahakama ya rufaa ya kimataifa ya
jinai, ICC, iliyoko Hague, Uholanzi imetupilia mbali rufaa
iliyowasilishwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Fatouh
Bensouda, ya kutaka mahakama hiyo kuishtaki Kenya katika kongamano la
kimataifa ya nchi wanachama wa mahakama hiyo.
Bensouda aliitaka
mahakama hiyo kuizomea serikali ya Kenya kuwa imekataa kushirikiana na
mahakama hiyo wakati ilipokuwa ikikusanya ushahidi dhidi ya rais Uhuru
Kenyatta.Aidha Bensouda aliliambia mahakama hiyo kuwa Kenya ilificha ushahidi ambao ungetumika dhidi ya rais Kenyatta.
Kukosekana kwa ushahidi huo ulisababisha kesi hiyo kusitishwa kutokana na ukosefu wa ushahidi na mashahidi wa kutosha.
Lakini majaji waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo wamesema kuwa mahakama ya chini ya ICC, ilifanya kosa kuwasilisha kesi hiyo kwa mahakama ya rufaa.
Majaji hao walisema mahakama iliyokuwa ikisikiliza kesi dhidi ya Kenya, haikuchunguza vyema maombi yaliyowasilishwa na mwendesha mashtaka, na hivyo kufanya kosa kuwasilisha keshi hiyo kwa mahakama ya rufaa.
Aidha majaji hao wamesema kuwa mahakama hiyo haihoji ikiwa masuala yote ya kisheria yalikuwa yametumika kabla ya kuamua ikiwa kenya itawasilishwa mbele ya baraza la nchi wanachama.
Wakati huo huo mahakama hiyo imesema kutokana na dosari hizo, rufaa hiyo imetupiliwa mbali na badala yake kesi hiyo kurejeshwa tena kwa mahakama ya chini ambayo kwa mujibu wa sheria ina mamlaka ya kuamua ikiwa Kenya itafikishwa mbele ya baraza hilo.
Majaji hao wa mahakama ya rufaa walisema wao hawana mamlaka ya kuamua kuishtaki Kenya mbele ya baraza hilo na kuwa uamuzi wa mahakama ya chini ulikuwa na dosari.
Bensouda alikuwa amewasilisha kesi kuitaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya Kenya kwa kukosa kushirikiana vyema na maafisa wa mahakama hiyo, wakati ilipokuwa ikijaribu kukusanya ushahidi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta, madai ambayo yalipingwa vikali na Kenya.
Kenyatta alifikishwa mbele ya mahakama hiyo ya Kimataifa ya Jinai, ICC, kwa tuhuma za kuhusika na ghasia na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2007-2008.
Lakini machi mwaka huu mahakama hiyo iliamua kufutilia mbali mashtaka yote dhidi ya rais Kenyatta baada ya mwendesha mashtaka kufahamisha mahakama hiyo kuwa hakuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo, kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha, na kuwa baadhi ya mashahidi wake walikuwa wameamua kutoshirikiana na mahakama hiyo.
Kesi hiyo dhidi ya Kenya sasa itasikilizwa upya na mahakama ya chini
No comments:
Post a Comment