30 August, 2015

Madhara ya kula Mayai yasipoiva vizuri kwa Afya

Mayai ni moja ya vyakula vyenye viini lishe muhimu kwa ajili ya afya ya mwili wa binadamu. Kwa kawaida mayai kabla ya kuliwa, huandaliwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchemshwa, kukaangwa au kuchanganywa na vyakula vingine kama vipande vya viazi mviringo ambavyo ni maarufu kwa jina la chips.

Pia, kuna baadhi ya watu wanaopendelea kula mayai mabichi kama dawa ya tiba mbadala, kwa ajili ya kulainisha sauti na wengine hupendelea kula mayai ya kukaanga ambayo hayakukaushwa vizuri.
Ukitembelea migahawa mingi utabaini kuwa watu wanakuwa na mitazamo tofauti na wanavyopenda kula mayai.

Mfano kuna wanaoagiza watengenezewe mayai kwa mtindo unaojulikana kama ‘macho ya ng’ombe.’ Ukiagiza namna hiyo, mpishi atataka kuuliza kama ni ‘macho ya ng’ombe’ ya kugeuza.

Ina maana kuwa ‘macho ya ngombe’ ya kugeuzwa ni yale yanayoivishwa pande zote lakini yale ambayo siyo ya kugeuza, huwa linaifa nusu. Upande mmoja unabaki ukiwa mbichi, na ndiyo raha ya baadhi ya watu.

Hata ukienda kwa wakaanga chipsi, utakuta wanawauliza wateja wao kama wanapokaanga na mayai wakaushe au wasikaushe. Hii inaashiria kuna watu wanataka wale chipsi zikiwa na mayai ambayo halijaiva sawasawa.

Kuna watu wengine wanaamini kwamba kula mayai mabichi kunafanya sauti inakuwa nyororo, hivyo wale waimbaji huwalazimu kufanya hivyo ili kufanya nyimbo zao zivutie.

Si hivyo tu, kuna baadhi ya watu huamini pia dawa ya kikohozi ni kunywa yai bichi lililochanganywa na asali. Hizi ni imani ambazo zimejengeka kwenye jamii na watu hufanya hivyo ili kufikia malengo waliyokusudia.

Katika siku za karibuni, imevuma kuwa mayai ya kwale yanatibu magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na kifua.

Katika mpango huo, wanapendekeza wahusika kula mayai mabichi ya kwale tena kwa kutafuna hadi kaka lake, yaani ganda la nje.

Hali hii imesababisha biashara ya mayai ya kwale kuwa kubwa na hata wafugaji wameongezeka mara dufu.

Wataalamu wanasemaje?

Baadhi ya tafiti za sayansi ya lishe na afya ya jamii, zinabainisha kuwa ulaji wa mayai katika hali ya namna ya ubichi, unaweza kuhatarisha afya.

Wakati mwingine, hali ya namna hii, huwa chanzo cha mlipuko wa magonjwa ya tumbo katika jamii. Katika milipuko ya magonjwa hayo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi hasa kwa watoto wadogo, wazee, wajawazito na watu wenye upungufu wa kinga mwilini.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba mayai mabichi yanaweza kusababisha maradhi ya kuharisha na homa ya matumbo kutokana na kubeba vimelea vya magonjwa aina ya Salmonella Enteritidis PT4. Vimelea hivi hatari kwa afya, vinaweza kuwa ndani ya yai au juu kwenye ganda la yai bila kuonekana kwa macho. Mgonjwa aliyepata uambukizo wa bakteria wa Salmonella kutokana na kula mayai, anaweza kuwa na homa kali, maumivu makali ya tumbo pamoja na kuharisha ndani ya saa 72 baada ya kula mayai.

Ugonjwa huu unaweza kudumu kwa siku nne hadi saba na baadhi ya watu huwa na hali mbaya kiasi cha kuhitaji matibabu ya kulazwa hospitalini.

Kwa baadhi ya watu ambao kinga ya miili yao si imara, vimelea vya Salmonella vinaweza kuingia katika mfumo wa damu na kusambaa mwili mzima. Jambo hilo linaweza kusababisha kifo kwa muda mfupi kama mgonjwa hatapewa matibabu sahihi na kwa haraka.

Nchini Uingereza ingawa, ugonjwa utokanao na kula mayai yenye uambukizo wa Salmonella umepungua sana, lakini angalizo la watu kuepuka ulaji wa mayai mabichi bado linadumishwa.

“Ni swala la kujua kwamba hatari bado ipo katika jambo hili, hata kama ni ndogo,” anasema Bob Martin ambaye ni mfanyakazi wa Wakala wa Viwango vya Ubora wa Chakula (The Food Standards Agency) nchini Uingereza.

Utafiti uliofanyika mwaka 2004-2005 katika maeneo mengi ya Ulaya ulibaini kuwa asilimia 20 ya mashamba makubwa ya kuku wa mayai, yalikuwa na kuku waliokuwa na uambukizo wa Salmonella. Hii ni kwa mujibu wa Richard Lawley katika makala yake yaliyochapishwa Februari mwaka 2013 katika tovuti ya Food Safety Watch.

Utafiti mwingine uliofanywa na Q.T. Bura na Henry B. Magwisha kutoka katika Wakala wa Maabara za Mifugo Tanzania (TVLA) kwa kushirikiana na profesa Robinson H. Mdegela wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), nao ulibaini kuwa ndege wengi wanaotaga mayai wana maambukizi ya vimelea vya Salmonella. Utafiti huo ulifanyika katika Jiji la Mwanza kati ya Desemba 2013 na Januari 2014.

Tukiachilia mbali uambukizo wa Salmonella, ulaji wa muda mrefu wa mayai mabichi au yale yasiyoiva vizuri hasa kwa akina mama wajawazito, unaweza kusababisha wazae watoto wanye ulemavu wa viungo vya mwili katika maumbile yao. Utafiti wa Lawrence Sweetman na wenzake uliochapishwa mwaka 1981 katika jarida la Paediatric toleo la 68(4), unabainisha kuwa ulaji wa mayai mabichi au yasiyoiva vizuri, unaweza kusababisha watoto wasiwe na nywele kichwani.

Utafiti wa Timothy D. Durance wa Chuo Kikuu cha British Columbia nchini Canada, uliochapishwa mwaka 1991 katika jarida la Sayansi za Vyakula (Journal of Food Sciences) toleo la 56(3), unabainisha kuwa ute mweupe wa mayai unaweza kusababisha upungufu wa Biotin mwilini.

Dr. Durance anaongeza kusema kwamba, ute mweupe wa mayai mabichi una protini aina ya avidin ambayo huzuia Biotin kusharabiwa (kufyonzwa) kutoka katika chakula kinapokuwa tumboni. Utafiti huo pia ulibaini kuwa hata mayai yaliyochemshwa au kukaangwa vizuri, bado ute mweupe huwa na Avidin yenye nguvu kwa asilimia 40.

Utafiti wa Profesa Hamid Said wa Chuo Kikuu cha California nchini Marekani, nao uliripoti kuwa ute wa mayai yasiyoiva, unasababisha upungufu wa Biotin mwilini. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la sayansi ya lishe katika tiba (American Journal of Clinical Nutrition) toleo la mwaka 2002. Utafiti mwingine ulioongozwa na Donald Mock na kuchapishwa katika jarida la sayansi ya lishe katika tiba la nchini Marekani toleo la 75(2) mwaka 2002, nao ulibainisha kuwa takribani asilimia 50 ya wanawake wajawazito, wana kiwango fulani cha upungufu wa Biotin mwilini hasa katika miezi mitatu ya mwanzo wa mimba.

Hali hii inafanya wajawazito wanaokula mayai mabichi au yasiyoiva vizuri katika kipindi hiki, kuhatarisha afya zao na za watoto wao walioko tumboni kwa kiasi kikubwa.

Utumiaji wa mayai ya namna hii kwa muda mrefu, pia unaweza kusababisha upungufu wa damu mwilini na ugonjwa wa mzio wa chakula hasa kwa watoto. Lakini pia utumiaji wa mayai yasiyoiva vizuri kwa muda mrefu, unaweza kusababisha ugonjwa wa kukatika katika kwa ulimi kutokana na upungufu wa vitamini B mwilini.

Hali ambayo husababisha shida wakati wa kula vyakula vyenye uchachu au vilivyokolezwa viungo vingi vya aina mbalimbali.

Tahadhari kubwa inahitajika wakati wa kuandaa mayai ili kuhakikisha kuwa chakula hiki muhimu hakigeuki kuwa chanzo cha madhara ya kiafya. Ni vizuri kutunza, kuchagua na kusafisha mayai vizuri kabla ya kuyachemsha au kuyavunja kwa ajili ya maandalizi mbalimbali ya mapishi.

Vyombo vinavyotumika kukorogea mayai mabichi ni lazima visafishwe kwa maji ya moto na sabuni kabla ya kutumika kwa ajili ya maandalizi ya chakula. Kwa namna yoyote ile mayai yasiliwe ikiwa hayakuiva vizuri au yanapokuwa katika hali ya ubichi.

Ni wakati kwa jamii kubadili mwelekeo kwa kula mayai ambayo yamepikwa hadi kuiva na kuepuka kula yakiwa mabichi.

Ni vyema pia ikaeleweka wapikaji wanapaswa kuwaelimisha wateja wao juu ya athari hizi ili kuwafanye wawe na uchaguzi sahihi wa vyakula watakavyotumia.


Katika jamii yetu, wapika chipsi huwa hawaoshi lile bakuli la kukorogea mayai kabla hayajakaangwa. Hii ni hatari kwa sababu chombo hicho kinaweza kikawa sababu ya kusambaza maradhi kwa watumiaji wa mayai.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...