21 August, 2015

Kikwete azijibu hoja za Ukawa

Tanzania's President KikweteRAIS Jakaya Kikwete, amesema Serikali yake iko imara ikijivunia utekelezwaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo na wote wanaosema nchi imemshinda, wanajidanganya kwa kufurahisha nafsi zao.

Alisema miezi michache kabla ya kumaliza muda wake, kumekuwa na uhuru mkubwa kwa watu kutoa maoni yao na wengine kupitiliza, lakini Serikali haipo tayari kuona mtu anatumia vibaya uhuru huo, kuleta machafuko na kuvuruga amani iliyopo nchini.

Hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walimtuhumu Rais Kikwete na kudai nchi imemshinda kutokana na umaskini mkubwa wa Watanzania.

Rais Kikwete aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora akitumia fursa hiyo kuwaaga na kusisitiza kuwa, haki za binadamu na utawala bora vikiheshimiwa, vitasaidia kulinda amani na utulivu wa nchi.

"Maneno ya wapinzani wetu kisiasa hayanisumbui, anayesema nchi imenishinda mpuuzeni, haijanishinda na wanajidanganya wenyewe, mimi sina wasiwasi na hilo lakini hatutakubali kuona mtu anatumia uhuru huo kuleta migogoro ya kidini au ukabila," alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, hata wale wanaosema nchi za Ulaya zina demokrasia ikiwemo Marekani, wajue hata huko sheria zao haziruhusu maandamano ya watu karibu na Ikulu, lakini hapa kwetu Tanzania, wanasiasa wanataka kuandamana Kariakoo wakiamini wana kundi kubwa la watu kumbe wengi wao ni vibaka wanaoiba bidhaa za wafanyabiashara.

"Ukitaka kuandamana, nenda Jangwani na ukiheshimu sheria ndio haki za binadamu zinapoheshimiwa, hata kama unayo haki lakini timiza wajibu upate haki," alifafanua Rais Kikwete.

Alisema katika utawala wowote, lazima kuwepo na uhuru na hilo kama halipo, watu wataidai kwa njia mbalimbali ili wapate haki yao, wakishindwa wanaweza kutumia bunduki kudai uhuru huo kwa kuwa msingi mkubwa wa amani ni haki.

Rais Kikwete alisema baadhi ya nchi zenye migogoro, chanzo kikubwa ni ukosefu wa haki; hivyo watu wanaweza kudai kwa mazingira ya kawaida na baadaye kupitia wanaharakati, nchi yoyote isiyo na haki za binadamu na utawala bora, si nchi tena bali ni msitu kwa sababu watu wanaweza kufanya lolote kwa wengine wasio na nguvu.

Migogoro ya ardhi

Akizungumzia migogoro ya ardhi, Rais Kikwete alisema lazima kuwepo mpango wa kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ambao wanapaswa kupunguza mifugo yao.

Alisema migogoro mingi ya ardhi inachangiwa na baadhi ya viongozi ambao si waaminifu kwa kuuza kiwanja kimoja kwa watu wawili au watatu huku wananchi wakiwa hawana elimu ya kutosha juu ya masuala ya ardhi hali inayowafanya wenye uwezo kutumia fursa hiyo kuchukua ardhi yao.

"Tumeshughulikia migogoro mingi ya ardhi, jambo hili hatuwezi kuliacha kwani kuna viongozi ambao ndio chanzo, tangu niingie madarakani kila anayetaka ardhi kubwa lazima niidhinishe.

"Maombi yote yaliyofika kwangu, niliagiza lazima Mkuu wa Wilaya katika eneo husika, aitishe mkutano na wananchi ili awaambie na wakikubali nami ndio naidhinisha kwa kutia saini," alisema.

Mauaji ya albino

Rais Kikwete alionesha masikitiko yake juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kutokana na ukatili wanaofanyiwa ukiwemo wa kukata viungo vyao kwa ajili ya imani za kishirikina.

"Inauma sana, wakati mwingine unachukia hadi unaamua kulala lakini tangu niingine madarakani, sijawahi kutoa idhini ya kunyonga zaidi ya kufungwa maisha, jambo hili kwa nchi yetu bado hivyo ni kazi yenu
tume kutoa elimu juu ya masuala haya," alisema Rais Kikwete.

Aliishukuru tume hiyo kwa kufanya kazi nzuri ya kutoa elimu inayohusu masuala mbalimbali yakiwemo mauaji ya albino kwani huwezi kuwatenga kwa kuwapa majengo yao, barabara zao hivyo lazima nao waishi kama wengine ndio maana wanachanganywa hata shuleni.

Mwenyekiti wa tume

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga, alisema kipindi cha miaka 10, imepokea malalamiko 26,818 ya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Alisema malalamiko 19,508 yalitolewa uamuzi na 7,310 yapo katika hatua za kupatiwa ufumbuzi ambapo hadi sasa kuna kesi 14 zilizopo mahakamani na tume inaendelea kufanya tafiti  mbalimbali katika
baadhi ya mikoa, kutembelea magerezani, kuangalia haki za wafungwa.

"Tunakushukuru sana Rais Kikwete, tunaviomba vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi nchini watende haki ili kulinda haki za binadamu, utawala bora, kuendeleza amani iliyopo," alisema.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...