Lowassa,
Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa CCM
mwishoni mwa mwezi uliopita na kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa fursa
ya kutimiza ndoto yake ya kugombea urais, akiwakilisha vyama vinne vya
Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.
Tangu ahamie
Chadema, Lowassa amekuwa akivuta wafuasi wengi kwenye shughuli za Ukawa,
hali inayoashiria uwezekano wa kuwapo kwa upinzani mkubwa kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Jana katika taarifa yake,
CCM haikutoa maelezo mengi kuhusu kamati hiyo zaidi ya kutangaza kuwa
itaongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana na kutaja majina ya
wajumbe.
“Hii ni kamati ambayo itakuwa inafanya
oparations za kila siku,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye wakati akitangaza kamati hiyo jana.
Kinana
anajulikana kutokana na kazi aliyoifanya ya kuongoza kampeni kwa
mafanikio, akifanikisha ushindi wa marais wawili mwaka 1995, wakati
alipoongoza kampeni za Rais Benjamin Mkapa na 2005 wakati Rais Jakaya
Kikwete akiingia Ikulu.
Licha ya Nape kutozungumzia
majukumu ya kamati hiyo, mmoja wa wajumbe, January Makamba alisema
wamejipanga vizuri na mwaka huu watafanya kampeni za kisasa.
“Tumejipanga
na namna tunavyojipanga ni siri yetu, ni mambo ya ndani ambayo sisi
wenyewe kwenye timu tunayafahamu na hatuwezi kutoa siri hizo kwa kuwa
ndizo silaha za maangamizi. Kwa kifupi tutashinda,” alisema naibu waziri
huyo wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia.
Makamba,
ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, alisema kampeni za CCM
mwaka huu zitakuwa za kisasa zinazoendana na mazingira ya kisiasa ya
msimu huu.
“Tumejitayarisha kushinda, juhudi zetu na ari yetu ni kushinda na kampeni zetu zitakuwa za kisasa zaidi,” alisema Makamba.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alitumia mfano wa mpira
wa miguu kuelezea ukubwa wa kamati hiyo dhidi ya wapinzani.
“Timu
hiyo ya kampeni ni sawa na kuileta Arsenal kuja kucheza na timu ya
daraja la tatu. Kwa hiyo katika hali hiyo usiulize matokeo,” alisema
Bulembo ambaye alikuwa mdau wa soka kabla ya kuingia kwenye siasa.
Kamati
hiyo ina wajumbe ambao walitemwa kwenye mbio za urais ndani ya CCM,
wajumbe wa Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond, wajumbe
ambao walikuwa kambi ya Lowassa alipokuwa kwenye mbio za urais ndani ya
chama hicho, wajumbe ambao ni maarufu kwa kurusha vijembe dhidi ya
wapinzani na wajumbe ambao walishaweka bayana uhasimu wao na mbunge huyo
wa Monduli.
Nape alisema Kinana atasaidiwa na makamu
wenyeviti wawili ambao ni Rajabu Luhwavi (Bara) na Vuai Ali Vuai
(Zanzibar) ambao pia ni manaibu wake kwenye chama.
Wajumbe
ambao ni wale waliotemwa kwenye mbio za urais ni Dk Asha-Rose Migiro,
Samuel Sitta, Mwigulu Nchemba, Dk Harrison Mwakyembe, Makamba, Lazaro
Nyalandu, Stephen Wasira, Bernard Membe na Makongoro Nyerere.
Pamoja
na kutopitishwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, makada hao wamekuwa
wakieleza kuwa hawawezi kuhama chama kama alivyofanya Lowassa na
watakuwa wakionyesha kuwa wamevunja makundi kwa kushiriki kumpigia
kampeni Dk Magufuli.
Kamati hiyo pia inamjumuisha
Sitta, Spika wa Bunge la Tisa ambaye anajulikana kwa kuruhusu mijadala
dhidi ya Serikali. Katika mijadala hiyo, Bunge lliliunda kamati
iliyoongozwa na Dk Mwakyembe kuchunguza sakata la Richmond
lililosababisha Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu.
Katika
hotuba yake ya kujiuzulu, Lowassa alidai kuwa suala hilo lilipikwa na
mahasimu wake wa kisiasa kwa sababu ya uwaziri mkuu.
Kundi
jingine la wajumbe wa kamati hiyo linahusisha makada waliokuwa kambi ya
Lowassa alipokuwa anawania urais kupitia CCM lakini hawakuhama naye.
Wajumbe hao ni Christopher ole Sendeka, Sadifa Juma Khamis, Shamsi Vuai
Nahodha na Sofia Simba, ambaye alipinga uamuzi wa Kamati Kuu wa
kupitisha majina matano na kuacha mengine kinyume na katiba.
Wajumbe
wengine ni Livingstone Lusinde, Abdallah Bulembo na Nape, ambao
wanajulikana kwa kushambulia wapinzani. Lusinde alijipatia umaarufu
katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, Machi 2012 alipoamua
kutumia lugha chafu dhidi ya viongozi wakuu wa Chadema.
Tayari
Kinana, Mwigulu, Nape, Bulembo na Wasira wameshanukuliwa wakirusha
mashambulizi makali dhidi ya Lowassa na wote waliohama CCM kuwa ni
makapi na mafuta machafu na kwamba Magufuli atashinda.
Vilevile,
wamo makada waliowahi kutangaza hadharani kuwa mahasimu wa Lowassa
tangu alipokuwa ndani ya CCM, akiwamo Anthony Diallo. Kundi jingine ni
la makada vijana kama Ummy Mwalimu, Steven Masele na Pindi Chana.
Wakizungumzia
uteuzi huo, baadhi ya wajumbe waliishukuru CCM kwa kuwaweka kwenye
kamati hiyo huku wakitamba kwamba watahakikisha chama hicho kinaendelea
kuongoza nchi.
Mwalimu ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Sheria na Katiba, alisema uteuzi wake ni jambo linaloonyesha kuwa
anaaminika na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi kuhakikisha CCM inashinda.
“Kamati imejipanga,” alisema. “Kazi kubwa ni kuhakikisha Dk Magufuli anashinda na anaingia Ikulu kwa kuwa anauzika.
“Hatutishiwi na kitu, tunaamini katika kushinda na kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunashinda kwa kupambana. Magufuli anauzika.”
Ahadi
ya kufanya kazi kwa bidii pia ilitolewa na Mbunge wa Kiembesamaki,
Waride Bakari Jabu ambaye alisema atajituma kwa asilimia 100 kuhakikisha
CCM inashinda.
“Nimefurahi na nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote kuhakikisha kuwa tunashika dola Zanzibar na Bara,” alisema.
Wakati Jabu akiyasema hayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Maua Daftari alitaka wananchi wawaunge mkono katika kazi hiyo.
“Hili
jukumu si la kwanza, lakini ninachoweza kusema ni kuwa wananchi
watuunge mkono ili tushinde,” alisema na kusisitiza kuwa watahakikisha
kampeni zinafanyika kwa usalama na wala si kwa fujo.
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Dialo alisema amepokea uteuzi huo na
anachosubiri ni kukaa na kupanga kitakachofanyika.
Makongoro,
ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), alisema hajapata
taarifa rasmi kuhusu kuteuliwa kwake kwenye kamati hiyo.
Hata
hivyo, alisema hiyo itakuwa ni mara yake ya pili kuwa kwenye kamati ya
kampeni kwani aliwahi kufanya kazi kama hiyo alipokuwa NCCR-Mageuzi
mwaka 1995. Alisema atazungumza zaidi kuhusu wajibu huo aliopewa pindi
atakapopewa taarifa rasmi na Nape.
Wakati Diallo na Makongoro wakisubiri kikao, Nchemba, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, alitumia nafasi hiyo kumsifu Dk Magufuli.
“Sisi
tunachokifanya ni kuweka njia tu ya kwa nini achaguliwe, kuwaambia
Watanzania kwa nini anafaa, kwa kuwa awamu ya tano ni awamu ya kazi tu,”
alisema.
....MWANANCHI
....MWANANCHI
No comments:
Post a Comment