Mabingwa wapya wa Ulaya klabu ya
FC Barcelona inajiandaa kumtangaza kiungo wa pembeni wa FC Sevilla,
Aleix Vidal kama ingizo jipya katika klabu hiyo baada ya kukamilisha
usajili wake siku ya jumamaosi.
Licha ya kuwa katika kifungo cha
kutosajili mpaka mwaka 2016, mabingwa hao wa Hispania na Ulaya wamekuwa
katika harakati za kunasa saini kadha wakadha kwa ajili ya kuboresha
kikosi chao ingawa watatakiwa kusubiri hadi Januari 2016 ili kuanza
kuwatumia wachezaji hao.
Aleix Vidal amesaini mkataba wa
miaka 5 na Barcelona siku ya Jumamosi baada ya klabu hizo mbili
kukubaliana juu ya ada ya uhamisho inayotajwa kufikia pauni milioni 10.
Winga huyo anayeweza kucheza pia
nafasi ya mlinzi wa pembeni, anatarajiwa kuwa nyongeza na mbadala sahihi
wa beki wa Kibrazil Dani Alves ambaye licha ya juhudi za raisi wa klabu
hiyo Josep Maria Bartomeu kumbakisha Camp Nou, anaonekana kuikaribia
milango ya Old Trafford na kufata nyayo za Victor Valdes aliyejiunga na
mashetani wekundu hao msimu uliomalizika.
Mhispania huyo aliyesajiliwa na
Sevilla msimu uliopita akitokea Almeria alikocheza michezo 120 na
kufanikiwa kupachika wavuni mabao 17, ameichezea Sevilla michezo 31
msimu huu na kufumania nyavu mara 4 huku akitengeneza mabao 11 na
kuisaidia vilivyo Sevilla katika mafanikio yake ya kombe la Europa msimu
huu.
Sasa Vidal atatambulishwa
rasmi siku ya jumatatu kwenye mkutano maalumu na waandishi wa habari
kama mchezaji halali wa wafalme hao wa bara la Ulaya baada ya kufaulu
vipimo vya afya.
No comments:
Post a Comment