MWANANCHI
Ilikuwa ni kama kutekeleza maandiko ya Biblia yanayosema “jifungeni nguo za magunia, ombolezeni na kulia kwa uchungu”, wakati ndugu walipokwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC kuchukua mwili wa marehemu. Walikuwa wamevalia magunia, lakini sababu ya
kuvalia nguo hizo haikuwa kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”.
kuvalia nguo hizo haikuwa kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”.
“Tumejiuliza
maswali mengi, tumeshindwa kupata majibu. Tumejiuliza tuvae nguo gani
hatukupata majibu. Kwa kuvaa hivi tunataka hao wauaji wajue damu hii
itawalilia popote walipo,” Beata Kiria, ambaye ni dada wa Victoria Sylvester aliyeuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kuzikwa nusu kiwiliwili.
Beata na ndugu zake walifika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kuuchukua mwili huo wakiwa wamevalia magunia.
Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa
4:30 asubuhi na saa 6:00 mchana wakati ndugu hao walipofika chumba cha
kuhifadhi maiti cha hospitali, huku baadhi yao wakiwa pekupeku na
kusababisha watu wengi waliokuwa eneo hilo pamoja na watumishi wa
hospitali kuwashangaa.
Wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia
maiti, ndugu hao walilia wakipaza sauti wakitaka wauaji wa mwanamke huyo
wakamatwe kabla ya kuchukua mwili na kuondoka nao.
Victoria (53), mkazi wa Kijiji cha
Masherini, Umbwe eneo la Kibosho aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa
kuamkia Ijumaa iliyopita na baadaye wauaji kuuzika mwili wake nusu na
kuacha kiwiliwili nje ya nyumba waliyokuwa wakiishi, jambo lililoibua
utata mkubwa ndani ya familia hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kiria alisema walichagua mavazi hayo baada ya kukosa vazi lingine.
“Tulitafakari
tuvae nguo gani ili kumuenzi marehemu lakini hatukupata jibu, ndiyo
tukaamua tuvae magunia kuonyesha kuwa waliomuua ndugu yetu thamani yao
inafanana na magunia haya,” Kiria.
Imezoeleka misiba mingi ndugu huvaa suti
nyeusi kwa wanaume huku wanawake wakivalia mavazi meusi au meupe ambayo
baadaye hujifunika na vitambaa vyeusi au vyeupe kwa akina mama.
MWANANCHI
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
amesema Kura ya Maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa
haitaendeshwa bila kuifanyia marekebisho sheria inayoongoza mchakato
huo.
Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida
Mashariki, alisema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya
Upinzani ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano) mjini hapa.
Kura ya Maoni ilipangwa kufanyika Aprili
30 lakini ikaahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kasi ndogo ya
uandikishaji wapigakura, lakini Lissu aliliambia Bunge jana baada ya
kuahirishwa kuwa hakuna uwezekano wa kura hiyo kupigwa bila ya kufanyia
marekebisho Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013.
Vikao vinavyoendelea mjini Dodoma ni vya
mwisho kwa Bunge la 10 lililochaguliwa mwaka 2010 na iwapo Serikali
haitawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, Kura ya Maoni
haitafanyika mwaka huu, kwa mujibu wa Lissu.
“Kwa
kifupi Mheshimiwa Spika, hakuna uwezekano kisheria wa kurudia tena hatua
zozote muhimu ambazo zilikwishachukuliwa kwa ajili ya kufanyika kwa
Kura ya Maoni iliyokuwa imepangwa Aprili 30, 2015,”Lissu.
“Mpaka
sasa Serikali hii ya CCM haijawasilisha muswada wowote wa marekebisho
ya sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni siku za usoni.
“Kama
ilivyokuwa kwa ahadi ya Kura ya Maoni ya Aprili 30, Serikali hii ya CCM
inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na Kura ya Maoni wakati kila
mwenye akili timamu anajua hilo haliwezekani bila kwanza kuwa na
mazingira wezeshi ya kisheria.”
Akiwasilisha hotuba ya upinzani, Lissu
alisema kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa, haiwezekani kuahirishwa wala
kuongezewa muda kama ilivyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Serikali.
Lissu alisema kitendo cha kutofuata muda uliowekwa katika sheria hiyo, kinaiondolea sheria hiyo uhalali wa kuendelea kutumika.
MWANANCHI
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad
amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni
30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo
mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali
Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na
ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi
hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za
Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na
matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha
Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano
wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za
Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya
kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema
ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa
ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi
unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa,
yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Profesa Assad alisema ofisi yake
ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na
kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika
migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33
bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold
Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili
msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
NIPASHE
Wakati mama mzazi wa watoto wawili
waliofariki dunia katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, akifunguka kwa
kusema kuwa anamwachia Mungu, Askofu wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, amesema tukio hilo ni ajali kama nyingine.
Mama wa watoto hao, Regina Saferi (32), amesema kwa kuwa Mungu ametaka iwe hivyo, hana la kufanya na anamuchia yeye (Mungu).
Kadhalika, Regina amesema kuwa haamini
kama vifo vya watoto wake vimesababishwa na utoaji kafara kama baadhi ya
watu wanavyodhani, lakini pia haamini kama kweli watoto wake walifariki
dunia kwa kupigwa na hitilafu ya umeme.
Alisema kuwa kama ni kweli walitolewa
kafara, wangefariki dunia na watoto wengine waliokuwapo wakicheza na
watoto wake. Alisema anaamini ni shetani aliyetoka nje ya Kanisa na
kutenda uovu huo.
Regina alidokeza kuwa siku moja kabla ya
kutokea kwa tukio hilo, aliota ndoto ya kutokea kwa msiba, lakini
hakujua utatokea wapi na utamfika nani.
“Niliota
ndoto, ilikuwa siku ya Jumamosi, niliota watu wengi wamekusanyika
katika msiba wakiomboleza, sikujua kama ndoto ile ilikuwa inanihusu mimi
na watoto wangu,” Regina akiwa katika hali ya huzuni.
Kwa mujibu wa Regina, haamini wala hakukuwa na mazingira ya kutokea kwa hitilafu ya umeme katika eneo hilo.
Alifafanua kuwa baada ya tukio la vifo vya watoto wake Sarah David na Goodluck David, kutokea watoto wengine walikwenda kucheza katika eneo hilo.
Alisema ni miaka minne sasa tangu aanze
kusali katika kanisa hilo na hajawahi kusikia wala kuona tukio la
kutokea kwa hitilafu ya umeme kanisani hapo.
Wakati Regina akisema kuwa anamwachia
Mungu, Askofu Gwajima amesema vifo vya watoto hao anavifananisha na
tukio la mtu yeyote ambaye atashika nyaya za umeme barabarani na
kufariki dunia.
Baba mzazi wa watoto hao, David Oturo,
alisema kuwa wanasubiri taarifa kutoka Jeshi la Polisi kabla ya
kuendelea na mipango ya mazishi.
Mwalimu wa darasa alilokuwa anasoma marehemu Sarah katika Shule ya Msingi Mirambo jijini Dar es Salaam, Asia Abdallah,
ameelezea kuhuzunishwa na kifo cha mwanafunzi wake Alisema Sarah
alikuwa ni mwanafunzi mwenye bidii darasani, hakuwa mtundu na alikuwa
anasoma kwa bidii.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni,
limetumia mabomu ya machozi kuwatawanya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar
es Salaam (UDSM), wanaoishi katika hosteli za Mabibo ambao walikuwa
wakiandamana kudai fedha zao za kujikimu.
Walichukua hatua hiyo kutokana na kucheleweshewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HELSB).
Tukio hilo lilitokea usiku walipoandamana kudai wawekewe fedha kwenye akaunti zao ambazo zimecheleweshwa kwa wiki 11.
Wanafunzi hao waliondoka Mabibo saa 4:00
usiku kwa maandamano kuelekea UDSM ili kuwashirikisha wenzao
kushinikiza uongozi kufatilia madai yao ndipo walipokutana na Polisi
waliolazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baada ya kushindwa
kutii amri ya kusitisha maandamano.
Katika purukushani hizo zilizodumu dumu
kwa saa tatu, Polisi walitumia mabomu mengi kuwatawanya wanafunzi hao
huku wanafunzi watatu wakikamatwa na wengine watatu wakijeruhiwa.
Licha ya kudhibitiwa na Jeshi hilo, jana wanafunzi hao waliendelea na mgomo wa kutoingia darasani mpaka watakapolipwa fedha zao.
Rais wa Serikali ya wanafunzi (DARUSO) Irene Ishengoma,
alisema maandamano hayo yalitokea baada ya wanafunzi kutangaziwa kuwa
watakopeshwa Sh. 20,000 na chuo kwa ajili ya kujikimu wakati wakisubiria
malipo yao.
“Baada
ya kusubiria kwa muda mrefu, uongozi wa chuo ulituahidi kutukopesha Sh.
20,000 kwa wanafunzi 7,000 ambao wanaidai HESLB tangu Mei 8, mwaka huu,
walipaswa kutuwekea fedha zetu,” alisema.
Alisema baada ya tamko hilo kutoka
Serikali ya wanafunzi, wanafunzi hao waligoma kupokea fedha hizo kwani
kiwango hicho ni kidogo.
Ishengoma alisema baada ya mvutano huo walikubaliana kutoingia darasani mpaka watakapolipwa madai yao.
Aliongeza kuwa walipozungumza na uongozi wa chuo waliahidiwa kuwa fedha hizo zitawekwa leo, hivyo walejee madarasani.
“Kwanini
tulipwe Sh. 20,000 wakati tunaidai bodi Sh. 450,000?” Hii haikubaliki
kwani hivi sasa maisha yamepanda na wanafunzi wengi wanaishi kuwa
kukopa,” alisema.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala, alisema amekutana na uongozi wa Daruso kujadiliana namna ya kutatua tatizo hilo.
NIPASHE
Serikali itaongeza mshahara wa watumishi wa umma kwa asilimia 13 .5 katika mwaka ujao wa fedha wa 2015/16.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Celina Kombani , alisema bungeni wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo.
Hata hivyo, alisema ongezeko hilo litapandisha mishahara ya kima cha chini zaidi huku cha juu kikiongezwa kwa asilimia 3.0.
Awali wabunge wakichangia bajeti yake
walitaka mishahara ikipandishwa iwanufaishe watumishi wa chini kwa vile
inapopanda kwa asilimia 10 mtumishi wa chini ambaye mshahara wake ni Sh.
265,000 anapata nyongeza ya Sh. 30,000.
Hata hivyo, kwa wenye mishahara inyoanzia Sh. 3,000,000 wanafaidika zaidi kwa nyongeza ya 300,000.
Kombani alisema wenye mishahara minono wanalipa kodi kubwa ya mshahara ya lipa kiasi unavyopata (Paye) kwa asilimia 30.
Kwa kutumia maelezo hayo mtu mwenye mshahara wa Sh. 3,000,000, atalipa Paye ya Sh. 900,000.
Akizungumzia ajira ya walimu alisema
taifa limeajiri walimu wa kutosha na sasa inajielekeza kwenye maeneo
mengine ya kilimo na afya.
Alisema mwaka unaoishia wa 2014/15 walimu walikuwa 31,000 wakati sasa wataajiriwa 28,957.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, alitaka sheria irekebishwe ili mawaziri wapewe pensheni.
NIPASHE
Rais wa Msumbiji Filipe Nyussi,
amewataka wabunge kuungana kupigana na vitendo vya ufisadi na ugaidi,
huku akisema serikali yake itaendeleza uhusiano uliopo kati ya nchi
mbili hizo.
Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania akiwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo kufanya hivyo tangu uhuru,
Rais Nyussi alisema: “Tumekuja
kujifunza demokrasia na namna ya kuendesha shughuli za bunge katika
masuala mbalimbali kama bajeti na kupigana na ufisadi.”
Aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kusaidia vita vya ukombozi kusini mwa Afrika na juhudi au ushiriki wake
wa kuzuia vita barani Afrika.
Alisema serikali yake itaendeleza uhusiano wa karibu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo.
“Sasa hivi tumeweza kushiriki chaguzi za kidemokrasia na ujumbe wangu hapa unawakilisha makundi ya watu mbalimbali kisiasa.
“Tumependa kuja kuona jinsi mnavyofanya kazi kwa uzalendo na mnavyoendesha nchi yenu kidemokrasia,” alisema.
Alisema bunge lina jukumu kubwa la kuwa
wawakilishi wa wananchi, hivyo akasema mbali na siasa, sasa wafanye kazi
ya kuendeleza uchumi, elimu, utalii na shughuli zingine kwa ajili ya
maendeleo ya wananchi na nchi yao.
Alisema serikali yake imefanya kazi
pamoja na bunge katika kupigana na ufisadi na kuandaa bajeti, lakini
wameona waje kujifunza kwa Bunge la Tanzania.
Aliomba ushirikiano wa mabunge ya nchi mbili hizo kwa kufanya kazi pamoja ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, aliwakaribisha Watanzania kuwa
huru kwenda Msumbiji na kufanya biashara au shughuli zingine za
maendeleo ili kuimarisha uhusiano uliopo.
Alisema katika kuimarisha uhusiano
uliopo kati ya nchi mbili hizo, serikali ya nchi yake imefungua milango
kwa Watanzania kwenda nchini humo kufanya biashara bila shida yoyote.
Katika hatua nyingine alitaka kuwapo kwa
utaratibu wa mabunge ya nchi mbili hizo kufanya ziara za mafunzo baina
yao ili kufanya kazi pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, alitoa angalizo kuhusu umuhimu wa
kuendeleza amani nchini kwa kila mmoja kuheshimu imani ya dini ya
mwenzake, huku akisisitiza kuweka kipaumbele kuhusu utaifa kwanza.
“Lazima tumuheshimu kila mmoja wetu licha ya tofauti zetu za dini, ila tukumbuke taifa letu ni muhimu zaidi,” alisema.
Alisema yeye na ujumbe wake wamerudi
tena katika nchi ya Nyerere na kukumbuka maneno ya unabii wake ya kutaka
nchi za Afrika kupigania ukombozi wa kiuchumi baada ya kupata uhuru wa
bendera, yaani wa kisiasa.
HABARILEO
Polisi Morogoro inamshikilia Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Boniface Jacob ,
mkazi wa Dar es Salaam kwa kudaiwa kukiuka Sheria ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, na ya Vyama vya Siasa nchini inayozuia uundaji wa
vikundi vya ulinzi wa vyama.
Kukamatwa kwa Jacob kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.
Jacob ambaye anajulikana kwa jina
maalumu la K5 alikamatwa kutokana na kudaiwa kukiuka utaratibu wa
matumizi ya kibali kilichoombwa na Chadema wilaya cha kufanya mkutano wa
hadhara na badala yake ukageuzwa kuwa ni wa kuhitimisha mafunzo maalumu
ya ulinzi kwa `Red Brigade’.
Hivyo alisema kiongozi huyo kwa kufanya
hivyo amekiuka sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 385 ,
inayokataza uundaji wa vikundi vya ulinzi kazi ya kuchukua jukumu la
Polisi .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa
kuwa vijana hao wamepatiwa mafunzo yenye malengo ya kutumia nguvu za
kijeshi licha ya katazo la vyama kuunda na kuwa na vikundi vya aina
hiyo.
Walinzi hao waliapishwa baada ya
kufanyika gwaride maalumu mbele ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
Chadema- Taifa, Wilfred Lwatakare, na kula kiapo cha utii kwa viongozi
wa chama hicho.
Akizungumza kabla ya kukamatwa kwake
katika tukio la uapishaji wa walinzi hao, Jacob alisema kikosi hicho
kina uwezo wa hali ya juu kukabiliana na matukio na ulinzi wa kura
pamoja na kikosi cha Poripori ‘ Kujificha porini’.
No comments:
Post a Comment