Ni vita kali kati ya timu yenye mafanikio zaidi Italia dhidi ya taasisi inayojiita “zaidi ya klabu”
– lakini timu hizi, Juventus na Barcelona, zitacheza fainali ya Ligi ya
Mabingwa mwaka huu jijini Berlin zikiwa na alama tofauti za kujivunia.
Miaka tisa iliyopita, Juventus
ilikuwa ikicheza katika Serie B (Daraja la chini baada ya lile la Ligi
Kuu ya Italia) baada ya kuadhibiwa kutokana na kuhusika kwao katika
kashfa ya upangaji matokeo (Calciopoli scandal). Wachezaji kama Gigi
Buffon, Claudio Marchisio na Giorgio Chiellini walikwepo wakati timu
ikiwa Serie B na sasa watakwepo katika mechi ya fainali, Berlin, Juni 6,
hawa wamekwepo tangu klabu ilipoanguka hadi kuzaliwa upya. Wachezaji
hawa wataingia kwenye mechi hiyo wakiwa na kumbukumbu za kusota kwenye ‘joto la jiwe’ hadi sasa wakiwa ‘ matawi ya juu’
Msimu wa 2006 – 07, Lionel Messi,
Xavi na Andres Iniesta walikuwa wakiichezea Barcelona kipindi hicho
ikiwa ni mabingwa watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa wakati wenzao,
Juve, walikuwa wakicheza dhidi ya timu kama Cittadella na Crotone. Hii
itakuwa fainali ya tatu ya Barcelona tangu msimu ule, ikiwa ni baada ya
kushinda fainali ya 2009 na 2011, baadhi ya mashabiki wa Barcelona
wanaamini kama sio ‘mbinu chafu’ za Inter ya Mourinho 2010, na ‘basi la Chelsea’ 2012, basi hii ingekuwa fainali yao ya tano ndani ya miaka saba.
Hakuna swali la nani ataingia kama mbabe kwenye fainali hii. Juventus itaingia kama ‘wanyonge’
(underdogs) uwanjani, hili ni jambo ambalo wao hawajalizoea kwa nafasi
yao. Barcelona inapewa nafasi kubwa hasa kutokana na uchezaji wao na
namna walivyofuzu kucheza fainali hii.
Barca itaingia ikiwa na kikosi chao cha ‘mauaji’
kikiwa na utatu unaoonekana kuwa mkali zaidi kuwahi kutokea katika uso
wa dunia – Messi, Luis Suarez na Neymar wamefunga jumla ya magoli 121
kati yao katika msimu huu – hii ikiwa ni tangu Alfredo Di Stefano, Paco
Gento na Ferenc Puskas waongoze safu ya ushambuliaji ya Real Madrid.
Kikosi cha Luis Enrique
kimetengenezwa na wachezaji waliozoea kushinda na wanaocheza kulingana
na utamaduni wa Barca, wachezaji ambao ‘hawatishwi na hali yoyote’ katika mechi kubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu duniani. Kama kutakuwa na hali yoyote ya ‘kwikwi’
basi hiyo itakuwa kwa wachezaji wapya kama Luis Suarez, Marc-Andre ter
Stegen na Ivan Rakitic. Lakini, tuache ukweli usemwe, hilo halionekani
kutokea hasa kutokana na muunganiko wao katika timu.
Juventus, yenyewe imejengwa na maveterani
pamoja na vijana wawili wakali walioonekana hawafai katika vilabu vyao
vya zamani: Alvaro Morata na Paul Pogba. Ambao wameshashinda medali
kadhaa kama watu binafsi. Carlos Tevez, Patrice Evra, Andrea Pirlo,
Morata na Buffon wote wameshacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa hapo
nyuma. Tofauti yao sasa ukilinganisha na Barca ni kuwa wameweza kufikia
fainali hii wakicheza pamoja kwa umoja kama timu wakati hapo zamani
waliweza kufika katika fainali huku wakiwa na wachezaji wenye majina
makubwa.
Tofauti nyingine kati yao na
Barcelona ni hii, wakati kikosi cha Barca kikionekana kitaendelea kuwa
pamoja na kusonga mbele, hilo haliwezi kuongelewa kwa Juve ambayo
wachezaji wao kadhaa wamekuwa wakitakiwa na vilabu vingine vikubwa
barani Ulaya. Jaribu kupeleka akili yako mbele misimu mitatu ijayo,
ukiondoa wachezaji kama Dani Alves na labda Javier Mascherano na Iniesta
(japo ni kama haiwezekani) wachezaji wao wote wanaweza kuendelea kuwa
pamoja Camp Nou.
Kwa bianconeri haiko hivyo. Real Madrid wana nafasi ya kumnunua tena (buy-back option) Morata huku Pogba akitazamiwa kuwa ‘bidhaa inayohitajika zaidi sokoni’ wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa, Juve kuzuia uhamisho wake haitakuwa rahisi.
Pia tukija kwenye suala lingine
la umri, Tevez ana miaka 31 na hajawahi kuficha matamanio yake ya
kumalizia soka lake nyumbani kwao, Argentina. Buffon ana miaka 38, Pirlo
35, Evra 33 na Stephan Lichtsteiner ana miaka 31. Kwa namna yeyote ile,
timu hii inahitaji kufanyiwa marekebisho angalau: ni vizuri kwao
kupunguza baadhi ya wachezaji hawa wakati huu ambao bado viwango vyao
vipo juu kabla nafasi hiyo haijapotea.
Tukiachana na vigezo vyote vya
kiufundi tulivyoviongelea hapo juu, upinzani mwingine wa aina yake
katika fainali hii huu hapa. Suarez atakutana uso kwa uso na wabaya wake
wa hapo nyuma katika nyakati tofauti, Evra na Giorgio Chiellini. Huku
katikati ya uwanja kukiwa na ‘vita’ ya aina yake kati ya ‘mafundi’ wawili wenye vipaji vya hai ya juu, Andres Iniesta dhidi ya Andrea Pirlo.
Pia hali nyingine ya kiushindani
itakuwa kati ya Neymar na Pogba, ambao wamepishana miezi 11 tu katika
kuzaliwa kwao, hawa wanatazamiwa kushika jukwaa la ushindani wa nani
bora duniani baada ya zama za Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kupita.
Buffon na Pirlo wanarudi kwenye uwanja ule ule walionyanyua Kombe la Dunia mwaka 2006.
Unahitaji stori zaidi? Tevez
atacheza dhidi ya Messi ikiwa hata mwaka haujapita tangu fainali ya
Kombe la Dunia, Brazil ichezwe ambayo walitakiwa waongoze safu ya
ushambuliaji ya Argentina pamoja, lakini Tevez aliishia kuangalia
fainali ile kwenye televisheni kwa sababu aliachwa kwenye kikosi cha
Argentina.
Hii ndio Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, itakayokuja kwako tarehe 6 mwezi wa 6. Tunza tarehe hii.
No comments:
Post a Comment