20 April, 2015

KAMA ULIPITWA NA MAGAZETI YA LEO JUMA TATU APRIL 20 NI ZAMU YAKO KUYAPITIA...

MTANZANIA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa adui yake namba moja ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha Alliance for Change and Transparance (ACT-wazalendo), Zitto Kabwe.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Furahisha Mwanza juzi, alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutokana na kile alichosema ‘ni adui kwao’.

Mtume Muhamad (S.A.W) alikuwa anazungumzia unafiki ambao una sura mbili na sifa zake, leo (ACT) wanasema wapo upinzani, wanasema msiunge mkono Ukawa halafu mnawakaribisha?
Nendeni kila mahali waambieni wananchi adui yetu mkuu ni Zitto. Sikilizeni niwaambie Taifa hili kama ni ufisadi tumeshazungumzia sana kuanzia EPA mpaka Richmond. Dk. Slaa (Willbrod) alipoingia bungeni aliyasema haya kwa sasa si mapya. Adui yetu ni Zitto na hatumtaki Ukawa,”Mnyika.
Zitto alisema pamoja na hali hiyo, ACT-Wazalendo haiko tayari kuzungumzia siasa za wakati uliopita kwa vile kufanya hivyo si afya njema kwa siasa za upinzani.
“Mwanzo walipotufukuza walituambia tukatafute vyama vingine hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa wakasema vipo kwa ajili ya kugawa upinzani tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuiondoa CCM…wenzetu pia hili hawalitaki sasa ni wajibu wenu kutambua watu gani hawataki kuiondoa CCM,”  Zitto.
Zitto ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira, waliwasili Mwanza saa 8.00 mchana na kupata mapokezi makubwa yaliyoanzia wilayani Misungwi.
MTANZANIA
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,amesema haogopi mtu yeyote wala kufa bali ataendelea kuinyoosha nchi anapoona haiendi sawa.
Kwa mujibu Askofu Gwajima, baadhi ya watu wamekuwa wakimhusisha kuwa na urafiki na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa jambo ambalo alikiri ni la ukweli kwa sababu walifahamiana tangu mwaka 1996.
“Niliwahi kumuita Waziri Mkuu Mizengo Pinda mara nne hapa ili aje azindue moja ya kazi zangu,hakuja badala yake nilimuita Lowassa na aliitikia wito wangu na kuja kuifanya kazi hiyo hivyo siwezi kumuacha.
“Wapo viongozi wengi ambao wanakuja kusali katika kanisa langu, kwa mfano Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Nape Nnauye, kwa nini wasimseme yeye badala yake wanamsema Lowasa tu?.
“Nashangaa mnatoka mlipotoka mnaongea kwa kubana pua, ukimuogopa mtu nchi itakuwa haiendi vizuri na mimi sitaogopa kukemea mambo ambayo hayafai katika jamii, mfano suala la Escrow.
Katika ibada hiyo aliliombea Taifa amani, uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kikao kijacho cha Bunge la Bajeti linalotarajia kuanzia baadaye mwezi ujao.
Wiki iliyopita, Askofu Gwajima alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mashitaka mawili ambayo ni kumtolea lugha ya matusi ambayo imemfedhehesha Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, na kuweka vibaya silaha anayomiliki.
MTANZANIA
Makada 20 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) wameonyesha nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Segerea.
Mbali ya makada hao, watu wengine 50 wamejitokeza kuwania nafasi ya udiwani katika jimbo hilo.
Kwa sasa mbunge wa jimbo hilo ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga aliyeshinda katika uchaguzi wa mwaka 2010 kwa kura 43,554 (asilimia 41.7) wakati mpinzani wake,Fred Mpendazoe alipata kura 39,150 .
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea, Gango Kidero alisema lengo ni kutetea maslahi ya wananchi ndani ya jimbo hilo.
Alisema licha ya makada hao kuonyesha nia,uamuzi wa mwisho upo kwa viongozi wa juu wa chama hicho kupitisha jina la mgombea mmoja baada ya Chadema kuungana na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).
Tuna zaidi ya watu 70 walioonyesha nia ya kuwania ubunge na udiwani wa Jimbo la Segerea lengo ni kulichukua kutoka mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi(CCM),” Kidero.
Alisema watangazania wote ni wasomi wazuri wenye fani mbalimbali na wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi ndani na nje ya jimbo hilo.
MTANZANIA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stephano Moshi (SMUCCO), Mchungaji Godfrey Malisa, ametangaza nia ya kugombea urais Oktoba mwaka huu kwa tikeki ya mgombea binafsi.
Mchungaji Malisa, alitangaza azma hiyo huku Serikali ikiwa bado haijaweka bayana kuwepo kwa mgombea binafsi kwa sababu Katiba Inayopendekezwa haijapitishwa.
Mwaka 2010, Malisa aligombea ubunge Jimbo la Moshi kwa tiketi ya
Chama cha Tanzania Labour (TLP).
Alisema ameamua kuchukua uamuzi huo ili kurejesha heshim Julius Nyerere.a ya taifa, kama ilivyokuwa imejengwa na na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu.
Hata hivyo, alisema enzi za Mwalimu Nyerere lilikuwa na heshima kubwa ndani na nje ya nchi ambapo tangu kuondoka madarakani hajaweza kupatikana kiongozi wa kuvaa viatu vyake.
“Mimi nimeishi Marekani na China…taifa letu lilikuwa linaheshimika, leo hii hata amani imeanza kutoweka kutokana na maujai ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ujambazi na wizi wa fedha za umma,” alisema.
MWANANCHI
Wezi wa vifaa vya magari jijini hapa wameunda mtandao mzito kama vile wana ‘serikali yao’ inayowalazimisha waathirika kuacha kutoa taarifa polisi badala yake kwenda kununua upya vifaa kwa wezi hao.
Licha ya wizi wa vifaa, kumekuwa na wizi mkubwa wa magari Dar es Salaam kiasi kwamba mwaka 2013, magari yaliyoibwa ni 400. Mwaka 2014 yaliibwa 375 na kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu magari 70 yameibwa.
Kutokana na hali hiyo, polisi jijini Dar es Salaam wamelaumiwa kwa kushindwa kutokomeza mtandao huo, licha ya wahusika kufahamika kwa majina, makazi na mahali wanakohifadhi vifaa hivyo vya wizi.
Hata hivyo, polisi nao kwa upande mwingine wametupa lawama kwa wananchi wanaoibiwa vifaa hivyo, kuwa hawatoi ushirikiano kwa jeshi hilo badala yake wameona njia rahisi ni kwenda kununua upya mali zao kwa wezi hao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya wananchi walioibiwa vifaa hivyo wanakataa kutoa taarifa polisi kwa kuhofia kupoteza muda, gari kubaki polisi kama kielelezo hadi vifaa vipatikane, kutakiwa kutoa fedha kwa wapelelezi au kuhisi kuwa baadhi ya askari wanahusika na mtandao huo.
Baadhi ya wakazi wa jiji waliowahi kuibiwa vifaa hivyo wamesema haichukui muda mrefu kwa mtu kubaini mahali vilipo na kuvipata tena, lakini kwa polisi wenye kila ujuzi kiupelelezi limeendelea kuwa tatizo.
Kutokana na uchunguzi wa gazeti hili, vifaa vinavyohitajika zaidi kwa sasa ni side mirror, control box, power window, vioo vya mbele na nyuma, taa, dash board, redio na baadhi ya vifaa vya injini.
Magari ambayo vifaa vyake vinaibwa zaidi ni yale yanayopatikana kwa wingi hasa aina ya Toyota na Suzuki, yakiwamo Escudo, Altezza, Mark II Grand, Cresta, Verossa, Noah, Ipsum, Klugger, Harrier, Vitz na Ist ambayo kutokana na wingi wake vifaa hivyo hupata wateja haraka.
Katika uchunguzi huo Mwananchi limebaini kuwa, watu wanaoharibikiwa magari, kugongwa au kuibiwa vifaa kwa siku ni wengi kwa hivyo wezi hupata uhakika wa kuuza vifaa hivyo.
Mkuu wa Upelelezi, Kanda ya Dar es Salaam, Constantine Massawe alipoulizwa sababu za kukithiri kwa tatizo hilo, alisema wizi wa vifaa vya magari unashughulikiwa kama uhalifu mwingine, lakini jeshi hilo halipati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi wanaoibiwa vifaa hivyo.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameitaka jumuiya ya albino nchini kuisukuma Serikali ili Rais Jakaya Kikwete asaini utekelezaji wa hukumu ya kuwanyonga wauaji wa albino.
Kauli ya Lowassa imekuja wiki moja tu baada ya Rais Kikwete kusema hajapelekewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya albino kutokana na mlolongo mrefu wa kisheria uliopo kabla ya kumfikia.
Rais Kikwete alisema hayo wakati wa ibada maalumu ya kuwekwa wakfu Askofu Liberatus Sangu kuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Hata hivyo, jana Lowassa aliyekuwa mgeni rasmi katika kampeni ya matembezi kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyoandaliwa na Klabu za Mbio za Pole ya Temeke na kushirikisha vikundi mbalimbali vya Dar es Salaam, alisema:
“Ninampongeza Rais Kikwete kutokana na jitihada zake za kukemea mauaji ya albino. Pia, nimesikia kuna watu sita wametakiwa kunyongwa lakini kwa maelezo ya Rais hukumu hizo hazijamfikia, hivyo nawaomba mfanye msukumo ili Rais asaini.
Kutokana na kukithiri mauaji hayo, Lowassa aliiomba Serikali kuunda kamati maalumu itakayokuwa ikichunguza mauaji ya walemavu hao bila kutegemea kamati za mikoa ili kuongeza ufanisi wa kuilinda jamii hiyo.
Mwanasiasa huyo anayetajwa kutaka kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, aliuambia umati uliokusanyika katika viwanja vya TCC Chang’ombe kuwa suala la ulinzi wa albino si la Serikali pekee bali la wananchi wote.
MWANANCHI
Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimemfukuza uanachama Mwanasiasa Mkongwe Hassan Nassor Moyo baada ya kubainika amekuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya chama ikiwamo kuhutubia mikutano ya hadhara inayoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) na kukejeli misingi ya Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imefahamika visiwani humo jana.
Uamuzi wa kumfukuza mwanasiasa huyo ulifikiwa jana na Kikao cha Halimashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi kilichofanyika katika Tawi la CCM Mbweni chini ya Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Yussuf Mohamed Yussuf ambapo wajumbe wote waliunga mkono ajenda ya moyo kufukuzwa uanachama wake.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Azziza Mapuri alisema kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao kujiridhisha kuwa Mzee Moyo alikuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyune na miiko na maadili ya chama.
Mapuri alisema kwamba uchunguzi uliyofanywa kuanzia ngazi ya Tawi Fuoni, Jimbo, Wilaya hadi Mkoa ripoti zote zimeonyesha Moyo alikuwa akivunja miiko na maadili ya chama kutokana na kitendo chake cha kuhudhuria mikutano ya CUF na kupanda katika majukwaa na kukejeli misingi ya mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kwa kutumia Ibara ya 93 (14) ya Katiba ya CCM Mzee Moyo tumemfukuza uanachama wa CCM baada ya kikao kupitia ripoti zote za uchunguzi na kujiridhisha alikuwa akivunja maadili na miiko ya chama chake,” Mapuri.
Alisema kwamba katiba ya CCM imeweka miongozo, maadili na kanuni na kila mwanachama wake anatakiwa kuheshimu, lakini Mzee Moyo ameshindwa kuheshimu na kufikia kukosoa chama hadharani badala ya kutumia taratibu za vikao vya chama.
Alisema kutokana na nguvu za kikatiba walizopewa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya mkoa kupitia kifungu cha 93 (14) cha katiba ya CCM, Mzee Moyo amefukuzwa bila ya kuhitaji baraka za wazee wa chama kwa vile ni utekelezaji wa katiba.
NIPASHE
 Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuondoa urasimu wakati wa kuandikisha wananchi kwenye daftari la kudumu la wapigakura ili watu wengi wajitokeze.
Pia ameitaka Nec kuweka dawati maalumu, ambalo litashughulika na kuandikisha vijana kwa lengo la kutaka wenye sifa za kujiandikisha wajiandikishe kwa wingi.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vijana zaidi ya 4,000 wa mazoezi ya ‘Jogging’, kutoka katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke baada ya kuhitimisha matembezi ya zaidi ya kilimita nane.
Matembezi hayo, ambayo yaliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahamn Kinana, yalilenga kuhamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Nape alisema ni vyema tume ikatambua kundi kubwa la Watanzania, ambao ni vijana kwa kuwapa vipaumbele vya kuwafanya wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Akizungumzia hofu ya kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Nape alisema haitawezekana na pia anatarajia tume itajipanga vyema kuhakikisha kila Mtanzania anajiandikisha.
HABARILEO
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umesema umeanza utambuzi wa Watanzania waishio katika maeneo ya hatari nchini humo kabla ya kuanza hatua za kuwaondoa na kuwarejesha nyumbani.
Hatua hiyo inatokana na kushamiri kwa mashambulizi yanayofanywa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya raia wa kigeni ambapo hadi kufikia jana watu sita wameuawa.
Taarifa zilizopo hata hivyo zinasema kwamba hakuna raia wa Tanzania ambaye ameuawa au kujeruhiwa katika vurumai hizo ambazo zimeanza Durban, Kwa- Zulu Natal.
Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, amesema kwamba Ubalozi Afrika Kusini umepeleka maofisa wake katika mji wa Durban kuangalia hali ilivyo.
Kasiga amesema kwamba serikali imeshatoa mwongozo wa namna ya kuwaondoa raia wake nchini Afrika Kusini.
“Utaratibu wa kuwaondoa Watanzania upo tayari, lakini itambulike kwamba si kila Mtanzania anayeishi Afrika Kusini ataondolewa bali wale walio katika maeneo hatarishi.
“Tutawaondoa Watanzania ambao wanaishi katika mazingira yaliyotishio au wale ambao mali zao zimeharibiwa,” alisema Kasiga akizungumza na gazeti dada Daily News kwa njia ya simu jana.
Alisema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye yuko nje kwa safari ya kikazi atatoa taarifa mara tu atakapowasili nchini.
“Kwa sasa waziri yupo nchini Jordan lakini atakuwa na nafasi ya kuzungumzia suala hili mara tu atakaporejea siku chache zijazo,” Kasiga.
JAMBOLEO
Wasomi na wananchi mbalimbali, wamemuomba  Rais Jakaya Kikwete, kutosaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 huku wakieleza kuwa kama utasainiwa watahamasisha wananchi kuupinga kwa kufanya maandamano ya nchi nzima mitaani.
Aidha, wamesema muswada huo ukisainiwa watatumia kama fimbo kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutokichagua katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Walisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo uliowashirikisha wananchi, wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu na wahadhiri wa vyuo vikuu kujadili athari za Sheria ya Takwimu  ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Wakati wa Bunge la 19 lilohitimishwa Aprili Mosi, mwaka huu, miswada hiyo iliwasilishwa na serikali bungeni kwa hati ya dharura na kupitishwa na Bunge na sasa hatua inayofuata utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuisaini ili iwe sheria ianze kutumika.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Kitilia Mkumbo, akizungumza katika mdahalo huo alisema miswada hiyo kama itasainiwa na Rais na kuwa sheria, itakuwa na athari kubwa kwa wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Profesa Mkumbo alisema kwa mfano, Sheria ya Takwimu ikianza kutumika itarudisha nyuma kupata wanafunzi wa PhD kwa sababu masomo yao yanategemea sana kupata takwimu.
Usalama mkubwa kuliko wote ni uhuru wa kupata taarifa, kutokupata taarifa sahihi kuna hatari,” alisema.
Profesa Mkumbo alisema Watanzania wanapenda kulalamika tu vijiweni lakini hawachukui hatua na kwamba katika suala la muswada huu kuna haja kwa wananchi kuandamana mitaani ili Rais asisaini.
Ndigwa Ezekiel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alieleza wasiwasi wake kama suala hilo likienda kupingwa mahakamani haki itatendeka kwa madai kuwa imeegemea upande wa serikali.
Wachangiaji wengine walisema kama miswada hiyo itasainiwa, hawataipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakati wa Mkutano wa Bunge, serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kueleza kuwa mtu akatayebainika kusambaza picha za ngono, miili ya watu waliokufa kwa ajali na usambazaji taarifa za siri za serikali, atatozwa faini ya Sh. milioni tano, kifungo kisichopungua miezi sita au vyote kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...