22 April, 2016

MISITU YETU TANZANIA TUNAFAIDIKAJE NAYO?

 
Kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na vyote vilivyomo tukiwamo sisi wanadamu, kwa mema mengi mno anayonitendea na hasa kwa kutujalia uhai hadi leo hii.
Kwa vyovyote vile bila ya Mwenyezi Mungu kutuwezesha na kututia nguvu sisi wenyewe hatuwezi, bali hali ilivyo ya kimazingira na kimaumbile tutakwama tu, hata hao wanaokwenda angani na kufanya wanayoyafanya huko si kwa uwezo wao tu, bali pia ni kwa mapenzi yake Mola

Nipende kuchua nafasi hii kukukaribisha katika makala yetu leo . Leo nitapenda kuzungumzia swala hili la Rasilimali ya Misitu tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Katika hali ya kawaida ni kwamba Misitu tulionayo inatosha kukidhi mahitaji yetu sote tuliopo karibu na Misitu katika mambo ya uhifadhi wa wanyama pori, kupata vyanzo vya maji, upatikanaji wa mbao kwa ajili ya ujenzi na hata kupatikana kwa kuni kwa ajili ya kupikia kwa wale wengi wetu tunayotumia nishati hii ya kuni.
 Misitu ya asili ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Mwenyezi Mungu tangu alipouumba ulimwengu, ikiwamo sayari hii tunayoishi sisi wanadamu. Kwa maneno mengine, misitu au maliasili zote tulizonazo ikiwa ni pamoja na madini, wanyamapori, samaki na viumbe wengine waishio baharini, ardhi (kwa maana ya udongo), maji (kwa maana ya vijito, mito, maziwa, mabwawa, bahari na ardhioevu), nishati mafuta na gesi asilia ni zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.
   Kwa bahati nzuri Tanzania Bara imebahatika kuwa na eneo kubwa lenye misitu ya asili pamoja na mapori mazuri yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori. Kwa takwimu za mwaka 1998 (ambazo sasa zimeboreshwa na matokeo ya mradi wa kitaifa wa kupima na kutathmini misitu ya asili), Tanzania ilikuwa na eneo la misitu ya asili la takribani hekta milioni 33.5.

Kati ya hizo, hekta milioni 13 ni eneo la misitu lililohifadhiwa kisheria (misitu ya hifadhi ya Serikali Kuu (Central Government Forest Reserves) takribani misitu 600 na misitu 200 ikimilikiwa na Serikali za Mitaa (Local Authority Forest Reserves) chini ya halmashauri za wilaya); na zaidi ya hekta milioni 20 ya misitu ya asili bado haijahifadhiwa na kusimamiwa kisheria.

Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, vijiji vichache vimeweza kutenga sehemu ya misitu katika vijiji vyao na kuitangaza kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji yenye jumla ya hekta zaidi ya milioni saba. Hatua hiyo ni ya kupongezwa maana vijiji husika sasa vina nguvu ya kisheria kusimamia na kutumia misitu husika ipasavyo na hatimaye kunufaika na usimamizi huo, kwa kuongozwa na Sheria ya Misitu na kanuni zake.
Vilevile, vijiji vinayo fursa ya kujiwekea sheria ndogo ndogo kwa lengo la kuimarisha zaidi utekelezaji wa shughuli za kulinda msitu kwa faida yao na Taifa kwa jumla. Pamoja na mafanikio hayo, bado sehemu kubwa ya misitu ya asili ambayo haijahifadhiwa kisheria inapatikana katika maeneo ya vijiji na haitumiki ipasavyo kuviletea vijiji maendeleo endelevu.

Miaka zaidi ya 20 Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Kutunza na Kuendeleza Misitu nchini (Participatory Forest Management-PFM). Dhana ya Ushirikishwaji ni mbinu ya uongozi inayowezesha kupata mchango wa mawazo na ushiriki mzuri kutoka kwa wadau mbalimbali, hasa katika utekelezaji wa shughuli za kujiletea maendeleo endelevu kwa kutumia rasilimali za asili tulizonazo.

Ushirikishwaji husaidia watu kubadilishana mawazo na kufahamu vizuri nini kinaendelea au kinatekelezwa kwa faida yao. Hivyo kwa kuwashirikisha wanavijiji katika masuala yanayohusu maendeleo yao vijijini ni suala muhimu sana na huondoa lawama, pia huongeza motisha wakati wa kutekeleza jambo lililoamuliwa.

Isitoshe, ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa anawajibika ipasavyo katika kutoa mawazo na kufikia uamuzi sahihi ili lengo na madhumuni ya mipango ya maendeleo katika sehemu yao iweze kufanikiwa. Ili wanakijiji au jamii katika ujumla wake waweze kufanya hivyo, ni lazima waelimishwe vya kutosha na kuwajengea uwezo (capacity) wa kusimamia na kutumia kwa misingi endelevu rasilimali na fursa zilizopo ikiwamo misitu ya asili.

Swali lililopo ni je tunafaidika vyema na hizi faida zitokanazo na misitu tulio nayo?
Zipo faida nyingi zitokanazo na Misitu hii tuliyo nayo na faida hizo na kama vile kutumika katika maswala ya ufugaji wa nyuki, hifadhi za wanyama, upatikanaji wa nishati ya kuni na upatikanaji wa mbao ambazo tunatumia katiaka maswala ya ujenzi na maendeleo hapa nchini.
Ni ukweli ulio wazi na usiopingika ya kwamba rasilimali hii haitufaidishi ipasavyo na nathibitisha ukweli huu kwa kutumia mfano mdogo tuu wa upungufu wa MADAWATI mashuleni mwetu hasa zile za msingi. Kimsingi tusingetarajia kuona fedheha na aibu hii kubwa inayotukumba  sisi leo hii Hapa nchini Kwetu. Kuna wakati nilikua natazama taarifa ya habari nikaona habari inayo onyesha watu wa Jamhuri ya watu wa SWITZILAND wakitoa msaada wa MADAWATI katiaka shule Fulani ya msingi huko Dar-es-salaam. Jamani hivi ni kweli tumekosa miti yakuweza kutupatia hayo madawati ambayo watoto wetu wanalizimika kukaa kwenye sakafu na juu ya mawe wakati wakiwa madarasani waifundishwa?
  Huo ni mfano mdogo tuu unaonyesha ni jinsi gani bado rasilimali za misitu hapa nchini hatufaidiki nazo ipasavyo.
Maoni yangu na mapendekezo yangu ni haya juu ya swala la ukosefu wa madawati mashuleni.
Kwa sasa zipa shule nyingi za UFUNDI hapa Tanzania ambazo zinamilikiwa na serekali na baadhi ya nyingine zinamilikiwa na taasisi binafsi na point ni kwamba Kuna baadhi ya misitu mikubwa ambayo imekomaa na ambayo inaweza kutupatia mbao kwa ajili ya kutengeneza madawati yakutosha.
Kwa nini serekali isivune miti hiyo kwa mujibu washeria na ki sha kutumia ile sera ya “KATA MTI PANDA MITI  ili kurudisha miti ambayo imevunwa kwa ajili yakutengeneza madawati?
    Inawezekana kabisa kufanya hivyo na kisha mbao kupatikana ambapo mbao hizo zitipelekwa katika vyuo vya ufundi ambapo wanafunzi wanaojifunza ufundi seremala watatengeneza madawati hayo kama sehemu ya  somo  lao darasani. Ni matumaini yangu kila mkoa vyuo hivi vya ufundi vinapatikana na jambo hili linaweza kufanikiwa kwa kiasi Fulani.
Serekali Kwa kupitia wataalamu wa mambo ya misitu waandae miche yakutosha kwa ajili yakupanda sehem zitakazokua zimevunwa miti hiyo.
 Kwakufanya hivyo tutaondoa aibu na tatizo hili la ukosefu wa madawati Katika shule zetu.
 Yasije yakawa yale yaPenye miti mingi hapana wajenzi.”
  Nichukue nafasi hii kukushukuru wewe ulie chukua nafasi na muda wako kupitia makala zetu. Tafadhali ungana nami tena katika makala zetu zinazotoka kila Mwisho wa wiki.
  
      MAKALA HII IMEANDIKWA NA:-
              Francis MawereNo comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...