15 March, 2016

Mahakamaa yatupilia mbali Pingamizi La Stephen Wassira

Mahakamaa Kuu Kanda ya Mwanza, imetupilia mbali maombi ya baadhi ya wapigakura wa Jimbo la Bunda Mjini ya kuruhusiwa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Makahama Kuu wa kufuta shauri lao la kupinga matokeo ya uchaguzi.

Maombi hayo yaliwasilishwa na Magambo Masato na wenzake wanne wanaompigania Stephen Wassira, wakiiomba mahakama hiyo kuwaruhusu kukata rufaa Mahakama ya Rufani baada ya kutoridhiswa na uamuzi ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana yaliyompa ushindi Ester Bulaya (Chadema), dhidi ya Stephen Wasira (CCM).

Jaji anayesikiliza shauri hilo namba 25 la mwaka 2016, Rose Ebrahim alisema jana kuwa anakubaliana na pingamizi lililowekwa na wajibu maombi kuwa hayana mashiko kisheria.

Pingamizi hilo lilowasilishwa na Wakili Mfawidhi wa Serikali, Paschael Marungu alidai aliyesaini hati ya maombi siyo aliyethibitisha kwani hilo ni kosa la kisheria.

Wakili Marungu alidai hati hiyo ilisaniwa na Wakili Denis Kahangwa na kuthibitishwa na Wakili Constantine Mutalemwa kwamba hilo ni kosa kisheria, hivyo kuiomba mahakama kutupilia mbali.

Akitoa uamuzi juu ya pingamizi hilo, Jaji Ebrahim alisema anakubaliana na pingamizi hilo kwani, makosa yaliyofanywa hayarekebishiki.

“Haya maombi nayatupilia mbali hayana miguu ya kusimamia, ni kosa kubwa hati kusainiwa na mtu mwingine halafu ikathibitishwa na mwingine, hakuna namna ya kurekebisha, lazima sheria ifuatwe na taratibu zake,” alisema.

Awali, Magambo na wenzake walifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga ushindi wa Bulaya, lakini ilitupiliwa mbali kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya sheria.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, Bulaya alipata kura 29,973 na Wasira wa CCM aliambulia 19,123 ikiwapo tofauti ya kura 10,000.
Hata hivyo, Wasira alilalamikia matokeo hayo akidai uchaguzi ulitawaliwa na udanganyifu. 
 
CHANZO: MPEKUZI HURU

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...