26 February, 2016

Rais wa Misri 'auzwa' mtandaoni

Sisi
Raia wa Misri wamekuwa wakimkejeli rais wao Abdul Fattah al-Sisi mtandaoni baada yake kusema kwamba anaweza kujiuza ili kusaidia uchumi wa taifa hilo.
"Ingeliwezekana mimi niuzwe, ningejiuza,” alisema Bw Sisi alipokuwa akihutubu kupitia runinga ya taifa.
Muda mfupi baadaye, ukurasa uliundwa kwenye mtandao wa kuuza bidhaa mtandaoni wa Ebay wa “kumuuza” Bw Sisi.
Kwenye ukurasa huo, uliofunguliwa dakika chache baadaye, mwuzaji alisema akiuza “jemedari ambaye amemaliza muda wake wa kutumia” na kuweka picha ya rais huyo hapo.
Bei ilizidi $100,000 (£72,000) baada ya saa kadha. Ukurasa huo baadaye ulifutwa.
Bw Sisi alikuwa pia amependekeza Wamisri watoe “pauni 10 ($1.2; £0.9) kwa Misri kupitia ujumbe wa simu” kusaidia kupunguza mzigo wa kiuchumi unaokumba taifa hilo.
Alisema hayo alipokuwa akizindua mpango wa ukuaji wa kiuchumi wa 2030.
Alikejeliwa pia kwenye Twitter huku watu wakifanyia mzaha tamko lake. Kwa muda, kitambulisha mada #Ebay kilivuma sana kwenye Twitter nchini humo.
Matatizo yanayokabili Misri kwa sasa ni pamoja na kupungua kwa uwezekaji kutoka nje pamoja na kupungua kwa watalii.
Kiwango cha mfumkko nchini humo kimepanda sawa na ukosefu wa ajira.
Hivi vimetokana na miaka kadha ya machafuko.
Bw Sisi ameapa kuendelea kujenga nchi hiyo “hadi mwisho wa maisha yangu au muhula wangu” na kuwahimiza Wamisri wamsikize yeye pekee iwapo wanaipenda Misri kwa dhati.
"Msiwasikize wengine, nisikizeni mimi,” amewahimiza.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...