10 August, 2015

Ugonjwa wa sukari ni chimbuko la chakula kisichofaa

Ni vigumu kujua aina ya chakula kinachokufaa, bila kujua jinsi mwili wako unavyokichakata. Kimsingi watafiti wamebaini makundi makuu matatu ya watu kuhusiana na jinsi miili inavyochakata chakula.

Chakula ambacho ni bora kwa mtu mmoja, kinaweza kuwa sumu baridi kwa mtu mwingine na kumletea madhara endelevu katika maisha yake. Kwa muktadha huu basi hakuna chakula bora kwa kila mtu. Chakula ni bora kwa mtu kama baada ya kukitumia mwili utakipokea vizuri, ukafyonza virutubisho na kikasaidia kuimarisha afya ya mlaji.

Ni vigumu kujua aina ya chakula kinachokufaa, bila kujua jinsi mwili wako unavyokichakata. Kimsingi watafiti wamebaini makundi makuu matatu ya watu kuhusiana na jinsi miili inavyochakata chakula.

Kundi la kwanza ni la wachakataji wa protini. Hawa miili yao inakubaliana zaidi na vyakula vya protini. Kwa watu wa kundi hili vyakula vya wanga na hususan vile vilivyochakatwa na kuchujwa kwa kiwango kikubwa (highly processed and refined), ni sumu baridi ambayo itawapelekea kuugua maradhi mengi ya kimfumo.

Kundi la pili ni la wachakataji wa wanga. Hawa miili yao inakubaliana zaidi na vyakula vya wanga. Kwa watu wa kundi hili la vyakula vya protini, hususan vile vilivyochakatwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuwa na muda mrefu wa matumizi, ni sumu baridi ambayo itasababisha kuugua maradhi mengi ya kimfumo.

Kundi la tatu ni la wachakataji wa vyakula vya protini na wanga kwa viwango sawa. Kundi hili kidogo lina bahati, kwa maana, halidhuriwi kwa wepesi na vyakula vilivyoko katika yale makundi mawili ya mwanzo.

Moja ya magonjwa yanayosababishwa na mkanganyiko huu katika kula ni ugonjwa wa kisukari. Mchakataji wa protini anapokula chakula cha wanga, kasi ya kuchakata wanga huo ni kubwa mno ikilinganishwa na mlaji mwenzake ambaye ni mchakataji wa wanga.

Kasi hiyo husababisha kiwango cha sukari kinachoingia katika mzunguko wa damu ndani ya muda mfupi kuwa kikubwa sana. Kutokana na hali hii kongosho hulazimika kufanya kazi ya ziada kuzalisha kiwango kikubwa cha kichocheo kinachojulikana kama insulini ili kuondoa sukari kwenye damu na kuipeleka kwenye seli ili itumike kutengenezea nishati.

Hali hii ikijirudiarudia, kongosho huchoka na kuanza kufanya kazi chini ya kiwango au wakati mwingine vipokezi vya sukari katika seli (receptors) hushindwa kuendana na kasi ya kuletewa sukari kwa ajili ya matumizi ya seli hivyo huishia kuikataa sukari hiyo.

Hali hii kitaalamu hujulikana kama insulin resistance, au pingamizi dhidi ya insulini kwa tafsiri isiyo rasmi. Kuna baadhi ya nyakati, vyote hutokea kwa wakati mmoja, yaani kongosho linafanya kazi chini ya kiwango, na pia mgonjwa anakabiliwa na pingamizi dhidi ya insulini.

Hivi karibuni imebainika kuwa moja ya sababu kubwa sana zinazosababisha vipokezi vya seli kushindwa kupokea sukari inayoletwa ni kitu kinachoitwa mfuro (inflammation). Mfuro ni uvimbe kama lengelenge hivi. Mfano wa mfuro ni pale unapojikwaa au kujigonga usoni na mwili ukaumuka na kutengeneza nundu.

Vichocheo vya kusababisha mfuro kwenye seli viko vingi lakini baadhi ya hivi ni vyakula tunavyokula kila siku. Vyakula hivi ni pamoja na sukari na wanga uiliochakatwa kwa kiwango kikubwa.

Athari za ugonjwa

Kisukarini ni ugonjwa ambao unasababisha mololongo wa matatizo mengine ya kiafya mwilini. Matatizo haya ni pamoja na uharibifu wa macho, unaotambulishwa na magonjwa kama glaucoma ambao husababisha uharibifu wa neva za jicho.

Matatizo mengine ni ugonjwa ujulikanao cataracts ambao unatokana na ukungu kwenye lenzi ya jicho na retinopathy unaosababisha uharibifu katika retina ya jicho.

Matatizo mengine ni ya miguu yanayotambulishwa na magonjwa kama neurapathy ambayo ni maumivu yatokanayo na uharibifu wa mishipa ya fahamu, vidonda sugu vya tumbo na gangrene ambao ni mkusanyiko wa tishu zilizokufa kutokana na kutofikiwa na mzunguko wa damu.

Matatizo mengine ni yale ya magonjwa ya ngozi na magonjwa ya moyo.

Mpango mzuri wa kuudhibiti ugonjwa wa kisukari ni kuufuatilia kwa makini. Hii ina maana kuwa ni muhimu kufanya kipimo kila siku, ikiwezekana hata mara mbili au tatu kwa siku. Kutokana na hali hii gharama za kuufuatilia ugonjwa huu ni kubwa na huathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kiuchumi ya mgonjwa.

Kwa mfano tu, hivi sasa katika zahanati na vituo vingi vya afya, gharama za kupima kisukari kwa mara moja ni kati ya Sh2,000 na Sh2,500.00. Unapomwambia mtu apime mara tatu kwa siku maana yake atumie kati ya Sh6,000 na Sh7,500.00 kila siku.

Ugonjwa wa kisukari kwa sasa kinaonekana kunyemelea hadhi ya kuwa ni janga la kijamii. Katika pande zote za dunia kisukari kinaongezeka badala ya kupungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), dunia inatarajiwa kuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 366 mwaka 2030 kutoka wagonjwa milioni 171 waliokuwepo mwaka 2000.

Mwaka 2000 Tanzania ilikuwa na wagonjwa 201,600 na mwaka 2030 inatarajiwa kuongezeka maradufu na kufikia 605,000. Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 66.7.

Hata hivyo janga la kisukari linaoonekana kuzikumba zaidi zile nchi ambazo raia wao wanapendelea mno vyakula vya wanga katika mitindo tofauti.

Vyakula hivyo ni soda, pasta, doughnut, keki, mikate, lambalamba, nakadhalika. Nchi kama Italy uwiano kati ya Wataliano wanaoumwa kisukari na wale ambao hawaumwi ni mtu mmoja kati ya 14. Inawezekana sababu kubwa ikawa ni ulaji wa piza, pasta na spaghetti. Hivi ni vyakula vinavyotengenezwa kwa ngano na Wataliano wanapenda kuvila kwa wingi.

Marekani uwiano wao ni mtu mmoja kwa kila watu 17. Hii nayo ni jamii ambayo inatumia soda, doughnut, chips, pizza, na vyakula vingine vya wanga vilivyochakatwa kwa kiwango cha juu. India uwiano wao ni mtu mmoja kati ya 39. Hawa nao ni mabingwa wa vitu vitamu. Wahindi wanapenda tamutamu za kila aina na sifa kuu ya vitu hivyo ni wingi wa sukari, ngano, mafuta na rangi.

Tanzania ina uwiano wa mtu mmoja kati ya 238. Huu ni uwiano mzuri sana ukilinganisha na nchi tulizotangulia kuzitaja. Sababu ya uwiano huu mzuri ni nini? Kimsingi sehemu kubwa ya Watanzania ni wala wanga zaidi kutokana na hali zao za kiuchumi?

Nadhani sababu kubwa ni ukweli kwamba Watanzania wengi ni wakaazi wa vijijini na kimsingi pamoja na kwamba sehemu kuwa ya chakula chao ni wanga, lakini kutokana na sababu za kiuchumi, wanalazimika kuula wanga huo katika mfumo ambao haujachakatwa.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...