MWANANCHI
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nanja, Kata ya
Lepruko, wilayani Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto wake wa kumzaa kwa
mtu mwingine kwa Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha magumu. Katika tukio hilo la kushangaza,
inadaiwa mwanamke huyo aliamua kumuuza mtoto huyo wa
kiume mwenye umri wa miezi minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
kiume mwenye umri wa miezi minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) Tawi la Arusha, Francisca Gaspar alisema walijaribu kumshawishi akamchukue mtoto wake, lakini aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu
aliyemnunua mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana
wadhifa mkubwa kijijini hapo.
“Kwa
kweli tulisikitishwa na kitendo hicho cha huyo mwanamke kumuuza mtoto
wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha magumu na ameshindwa kumlea,” Samsoni.
Alisema walimwita mwanamke huyo kwenye
ofisi ya kitongoji na kumhoji sababu zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini
aliwaaambia kuwa hana uwezo wa kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema
watahakikisha wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini
tumeambiwa kuwa mama huyo ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa
hapa kijijini na hajulikani aliko mpaka sasa.”
MWANANCHI
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo jana
alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba
wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari
iliyomkariri Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo,
hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada
ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na
unywaji wa pombe haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la
Kikelelwa lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa
ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja
Kikelelwa kama eneo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia
mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na
kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa
ajili ya tendo hilo,” Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya
wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya
kukamata pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili
zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa
hizo akidai kuwa siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na
ulevi huo au wanawake wote.
“Hiyo
kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume wangapi Rombo wana
tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida hiyo. Siyo
sahihi kutoa kauli ya jumla,” .
MWANANCHI
Ushauri unaotolewa mara kwa mara kwa
Serikali, taasisi zake na mashirika ya umma umekuwa ukipuuzwa na
kusababisha Serikali kuendelea kupoteza fedha nyingi kwa njia ya ufisadi
huku Deni la Taifa likizidi kukua, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi
maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti ya CAG imeweka bayana ufisadi wa
takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo
hayana maelezo ya kutosha na ripoti hiyo maalum inaonyesha kuwa uovu huo
umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya
upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa uchanganuzi wa Mwananchi,
Sh600 bilioni zilizofanyiwa ufisadi, zingeweza kusaidia kupunguza nakisi
kwenye bajeti ya Serikali kwa kuelekezwa kwenye wizara tatu ambazo ni
Ofisi ya Rais, iliyopangiwa Sh587 bilioni, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
(Sh68.8 bilioni) na Ofisi ya Makamu wa Rais (Sh112 bilioni).
Pia, fedha hizo zingeweza kujenga vyumba
8,000 vya madarasa kwa gharama ya Sh75 milioni kila kimoja au kuwezesha
vijana zaidi ya mara 12 ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete,
au kujenga kilomita 600 za barabara kwa kiwango cha lami.
Ukaguzi huo maalumu ulifanywa ili
kuangalia kama rasilimali zilizotengwa zimetumika kwa ufanisi kwa
kuzingatia kiwango cha fedha kilichowekezwa, tija na ufanisi kama
ilivyotarajiwa na kupitishwa na Bunge kwenye maeneo kadhaa, inaeleza
ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapendekezo
ya CAG yalitolewa katika ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi za miaka ya
nyuma kwenye maeneo ya usimamizi wa udhibiti wa athari za mafuriko kwa
Serikali, mikoa na serikali za mitaa uliofanyika kwa kutumia mafuriko
yaliyowahi kutokea Babati (2007).
Sehemu nyingi za matokeo ya uchunguzi
kwenye ripoti hiyo zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG
ulifanywa chini ya asilimia 50.
MWANANCHI
Baada ya vifo vya wakimbizi kutoka Burundi kufikia 40, Serikali
imelazimika kuongeza idadi ya kambi za wakimbizi ili kupunguza
msongamano Nyarugusu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga alisema jana kuwa hali iliyopo kwenye Kambi ya Nyarugusu siyo ya kuridhisha.
Alisema wakimbizi waliopo kambini ni 29,145 na ambao hawajaingia wakiwa katika uwanja wa Lake Tanganyika ni 4,729
Nantanga alisema Serikali imelazimika kuongeza kambi moja katika eneo hilo litakaloitwa Nyarugusu 2.
Alisema wameshaanza kuwahamisha wakimbizi kutoka kwenye uwanja huo chini ya uangalizi mkali.
“Tumebaini wakimbizi wanabanana
sana kwenye kambi moja, kuna wengine wajawazito, wagonjwa wa
kipindupindu, hivyo tumelazimika kuongeza kambi ya pili,” Nantanga.
Alisema Serikali inashirikiana na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuhakikisha huduma za chakula na matibabu zinapatikana.
Nantanga alisema kuhusu suala la ulinzi, Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna uhalifu wowote utakaotokea kambini hapo.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe
alisema wanashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhakikisha
wanapeleka timu ya wataalamu maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kufanya
tathmini na kutoa elimu ya afya.
MWANANCHI
Wakazi wa Mji wa Njombe, jana walikumbwa
na taharuki kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa na Polisi kwa
lengo la kutawanya waandamanaji waliokuwa wanapinga mauaji ya mkazi
mmoja anayedaiwa kupigwa risasi na askari na mwingine kujeruhiwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Franco Kibona alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia tuhuma hizo wakati hali ya kiusalama haijatulia.
Kamanda Kibona aliyekuwa eneo la tukio, aliwasihi wananchi kutulia kwani madai yao yanashughulikiwa.
Mauaji hayo yaliyotokea juzi usiku wakati wakazi hao wawili walipokuwa kwenye klabu ya pombe ya Nyondo, Mtaa wa Kambarage.
Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa
aliyeuawa ni Basil Ngole na majeruhi ni Fred Sanga ambaye amelazwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe.
Wakazi hao walikusanyika hospitalini
hapo saa moja asubuhi, huku wakipaza sauti za kulitaka Jeshi la Polisi
kugharamia mazishi ya marehemu pamoja na matibabu ya majeruhi.
Kutokana na kadhia hiyo, polisi walifika
eneo la tukio na kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu na kusababisha
mmoja ambaye ni dereva wa bodaboda kujeruhiwa.
Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wananchi ambao waliziba barabara, kwa mawe, na kuchoma magurudumu ya gari.
Majeruhi Sanga akizungumza kwa tabu
akiwa hospitalini alisema wakati akiwa katika klabu hiyo, askari wa
doria ambao walikuwa hawajavaa sare walifika eneo hilo na kuwaweka
wateja chini ya ulinzi.
Alisema hali hiyo ilizua mzozo, ndipo walipolazimika kufyatua risasi ambazo zilimpata yeye na mwenzake aliyefariki dunia.
Mkazi mmoja wa Njombe, Emanuel Filangali alisema kitendo cha baadhi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya raia ni cha kulaaniwa.
Alisema kuwa inadaiwa kosa la marehemu na majeruhi ni kunywa pombe nje ya muda katika klabu hiyo.
NIPASHE
Mtu mmoja amefariki dunia baada ya
kuanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha kwenye
Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia mpya ya Biometric Voters Registration (BVR).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi
saa 6:30 mchana kwenye kituo cha Lusyoto, kata ya Mpuguso katika eneo
la Ushirika, wilayani Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza
uandikishaji wa wapigakura wilayani humo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa ni Mary Kabejela anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya
mashuhuda walisema Mary akiwa kwenye mstari wa foleni ya kuelekea kwenye
chumba cha uandikishaji, ghafla alionyesha kudhoofika na kuishiwa nguvu
na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja wa mashuhuda wa
tukio hilo alisema baada ya mama huyo kuanguka, wananchi walimwinua na
kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana, ambako alipoteza
maisha wakati akipatiwa matibabu.
“Tulimwona
akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo tulipomwinua na
kumpakia kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini wakati daktari
akianza kumhudumia alifariki dunia,” Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa
kisiasa waliozungumzia tukio hilo, walisema kifo cha mama huyo huwenda
pia kimechangiwa na kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na
kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye
ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa Kamanda Msangi
amesafiri kikazi na kwamba kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia alikuwa nje
ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwambigija,
maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, ambaye yupo wilayani Rungwe kama
wakala wa chama chake kwenye kazi hiyo, alisema uandikishaji unafanyika
kwa kasi ndogo, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda
mrefu na hata kusababisha presha kuwapanda.
“Inawezekana huyu mama akawa amekufa
kutokana na presha kupanda, kwani alisimama kwenye foleni tangu asubuhi
huku akipigwa na jua kali, kutokana na umri wake kuwa mkubwa huenda
presha ilimpanda na kumpelekea kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya uandikishaji siyo nzuri
kutokana na watumishi wa serikali waliopewa kazi hiyo kuonekana kama
wanajifunza hivyo kutumia muda mrefu kukamilisha kumwandikisha mtu
mmoja, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo la kifo, zoezi la
uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura lilianza
juzi kwa kusuasua wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba mtandao
ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa siyo mzuri, idadi
kubwa ya vituo vya kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza
uandikishaji hadi saa 4:00 asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rungwe, Veronica Kessy, alikiri kuwapo kwa changamoto katika siku ya
kwanza ya uandikishaji, ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo tatizo hilo lilikuwa
la muda mfupi na baadaye hali ilikuwa nzuri na kasi ya uandikishaji
ikaendelea vizuri kama lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni vituo vichache tu
ambavyo zoezi la uandikishwaji wapigakura liliingia dosari kwa kukumbwa
na changamoto ndogondogo kama vile kuchelewa kufunguliwa, kujitokeza kwa
idadi kubwa ya wananchi kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo la
mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya
zoezi la uandikishwaji lilianza juzi katika kata 10 zilizopo ndani ya
Bonde la Uyole, ambako liliendelea vizuri licha ya wananchi kulalamikia
kasi ndogo ya waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye kulitaka
kutokea tafrani baada ya wananchi kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa
kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha
kuandikishia wapiga kura akiwa na daftari na kalamu akiorodhesha watu
wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia juu mtu huyo
wakitaka kumpiga kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati na
kumwondoa kwenye eneo hilo kabla hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya uandikishaji katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma na Tabora
utaanza leo, huku Katavi ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza ilihusisha mkoa wa
Njombe ambayo ulikamilika katikati ya Aprili, wakati awamu ya pili
inaendelea katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.
Uandikishaji huo umekuwa ukilalamikiwa
kusuasua kutokana na kasoro kadhaa hususani uchache wa vifaa (BVR kit),
uchache wa waandikishaji na vifaa hivyo mara nyingi kukwama kufanya
kazi.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amesema
atahakikisha anasaini miswada miwili ya habari kabla ya kumalizika kwa
mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti unaendelea.
Miswada hiyo ni wa sheria ya kupata habari na wa sheria ya vyombo vya habari huku.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati
akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu uwajibikaji na uwazi katika
serikali, jana jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mbele ya
washiriki wa mkutano huo takribani 200 kutoka nchi 65 ambazo ni
wanachama wa mpango huo wa kidunia wa kuendesha serikali katika
uwajibikaji na uwazi (OPG), wakati akielezea mafanikio yake katika
kukuza demokrasia na uwazi kupitia maeneo mbalimbali yakiwamo uhuru wa
habari na matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Tayari miswada ya habari imeshapelekwa
bungeni, ilishapelekwa kwa mara ya kwanza. Ni matumaini yangu wabunge
wataijadili kabla ya kumalizika kwa vikao vya bunge la bajeti
linaloendelea mjini Dodoma ili nami niweze kuisaini katika muda wangu
uliobaki,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, Rais Kikwete, hakueleza
namna wadau wakiwamo waandishi wa habari watakavyoshirikishwa katika
utoaji wa maoni kuhusu miswada hiyo kabla ya kusainiwa kuwa sheria.
Miswada hiyo ilipelekwa bungeni kwa hati
ya dharura katika mkutano wa 19, lakini wadau walipinga wakisema
serikali ilikuwa na nia mbaya.
Hata hivyo, baada ya wadau kukutana na
Spika, Anne Makinda, Spika aliirejesha miswada hiyo kwa Kamati ya Huduma
za Jamii ili ipitishwe kwa utaratibu wa kawaida ili kuwapa fursa wadau
kushirikishwa.
Alipiulizwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashililah, ili kuthibitisha iwapo miswada hiyo kwa mujibu wa kanuni za
kibunge imo katika ratiba kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano wa
bajeti, hakuwa tayari kulizungumzia jana.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Saidi Mtanda, alisema tangu kumalizika mkutano wa 19, kamati yake
haikupokea miswada hiyo kwa ajili ya kuanza utafutaji wa ,aomi ya wadau.
NIPASHE
Wakati vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikianza kesho, mwanasiasa mkongwe, Amina Salum Ali,
amekuwa mwanamke wa kwanza wa daraja lake ndani ya chama hicho
kutangaza wazi nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wanawake wamekuwa wanyonge
kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni
wakati mwafaka kwao kujiamini katika jamii kwani uongozi siyo fedha bali
ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.
“Nimeona
nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi yangu katika
uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi, mafuta,
kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika kuwaongoza
Watanzania wenzangu kwa kushika nafasi za juu,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.
Amina ambaye aliwahi kushika nafasi za
juu za uongozi Zanzibar na Tanzania Bara, ukiwamo uwaziri wa fedha
Zanzibar, alisema serikali inatambua mchango wa wanawake katika jamii
hivyo kupewa nafasi kubwa kama vile ujaji na uhakimu ili kuongeza zaidi
ufanisi wao kiutendaji.
“Wanawake
wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za juu za uongozi
kwamba kunahitaji fedha hivyo wanaishia kuwa wanyonge. Siyo kweli,
wajitokeze kwa wingi ili kitimiza ndoto za kuwajibika kwa taifa letu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wanawake
wamepigana sana dhidi ya mfumo dume na kwamba baada ya miaka 20 ya
maazimio ya Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika mjini Beijing,
China mwaka 1995, hali kwa sasa imebadilika na wanawake wanapewa nafasi
mbalimbali za uongozi.
Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda
mwanamke, lakini mfumo dume umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama
haijafikia asilimia 50 kwa 50.
“Jambo
kubwa kwa mwanamke ni kujiamini katika mambo yote… wanawake wa Tanzania
hatuna utaratibu wa kuchangiana katika harakati za uchaguzi. Utaratibu
wa mwanamke kupata fedha za mitaji kwa hapa nchini bado mgumu hasa
katika mabenki lakini tusiogope. Mimi nina amini ninaweza kuiongoza
jamii yetu,“ Balozi Amina.
Balozi Amina ametangaza ni ya kuwania
nafasi hiyo kubwa kuliko zote nchini wakati kesho vikao vikao vya juu
vya maamuzi vikitarajiwa kuanza kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa
uteuzi wa wagombea wa CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge
na urais Oktoba, mwaka huu.
NIPASHE
Mashabiki wa ngumi kutoka sehemu mbalimbali duniani wameliita pambano la ngumi baina ya Mayweather na Pacquiao kuwa ni la kitapeli na wametaka warudishiwe pesa zao za ziada.
Kesi zipatazo 32 zimeshafunguliwa nchini
Marekani zikieleza kwamba Pacquiao alipaswa kubainisha kuwa ana jereha
lake la beka kwa mashabiki wake kabla ya pambano hilo ambalo Mayweather
alishinda kwa pointi za majaji wote watatu baada ya raundi 12 ambapo
mashabiki wengi wanaona hazikufanana na promosheni ya pambano lenyewe.
‘Pambano la karne? linaonekana kabisa ni utapeli wa karne, mashitaka hayo yameeleza.
‘Halikuwa pambano zuri wala la kuburudisha, halikuwa na ushindani, lilikuwa linaboa, la taratibu mno na halikuwa na mvuto’…
Mashitaka yalifunguliwa kwa niaba ya baa ya Flights beer
iliyolipa kiasi cha milioni 5.2 kwa ajili ya kuonyesha pambano hilo,
baa iliyokuwa karibu na uwanja wa ndege wa Los Angeles na imesisitiza
kitendo hicho ni sawa na wizi wa wazi.
HABARILEO
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
amewaomba radhi wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini, kwa kuchelewa
kuwafikishia fedha zao za kujikimu. Hata hivyo, aLIsisitiza kuwa tangu
juzi fedha hizo zilishatoka Hazina.
Akizungumza bungeni janaalipokuwa akitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya
(CCM), Mwigulu aliagiza taasisi zinazohusika kuacha shughuli zote,
ikiwemo vikao ili kuhakikisha fedha hizo zifike kwa wanafunzi hao jana.
“Serikali
imeshatoa fedha, naagiza taasisi zipeleke fedha hizo leo hii hii ili
wanafunzi wasome tupate wataalamu wazuri…hii haitatokea tena,” Nchemba.
Awali, Bulaya aliomba Mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o
na alipopewa nafasi, alisema wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), wamegoma kwa kuwa hawajapelekewa fedha hizo na hawana
ugomvi na kitu kingine.
Kwa mujibu wa Bulaya, wanafunzi hao
wanaipenda Serikali yao, lakini kuchelewa kwa fedha hizo, kumesababisha
mateso kwa wanafunzi hao ambao wengi ni watoto wa masikini wanaotokea
vijijini, huku wanafunzi wa kike wakiathirika zaidi.
Bulaya alisema hata jana alipokuwa
akizungumza bungeni, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Dar es Salaam,
kilikuwa kimefikia uamuzi wa kurejesha nyumbani wanafunzi wote wa mwaka
wa kwanza, kutokana na uchelewaji wa fedha hizo na kutaka Serikali
ieleze kwa nini imechelewesha fedha hizo.
Alisema kwa utaratibu huo mpya,
iliamuliwa kuwa fedha zinazotakiwa kwenda katika mifumo rasmi, ziwe
zinapewa kipaumbele kwa kupelekwa kwanza kabla ya maeneo mengine ili
uchelewaji wa fedha hizo usitokee tena.
Wanafunzi hao waligoma kuingia
madarasani kuendelea na masomo juzi na kufanya mkutano chuoni hapo,
kushinikiza Serikali kuwalipa fedha zao za kujikimu.
Kwa mujibu wa mkataba kati yao na Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, fedha zinatakiwa kulipwa wiki ya
8 baada ya kusainiwa kwa mkataba baina yao na Serikali, lakini mpaka
juzi ilikuwa wiki ya 11 bila malipo hayo.
Wanafunzi hao walisema hawana nia ya
kufanya fujo za aina yoyote, bali wanachohitaji ni kupata suluhu ya
tatizo hilo, ambalo limewaathiri kimasomo na kisaikolojia.
Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Shitindi Venance,
alinukuliwa akisema kuwa matatizo hayo yanatokana na mfumo mbaya wa
mamlaka yenye dhamana ya kukusanya fedha za mikopo kwa walioajiriwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala alikiri madai ya wanafunzi hao 7,000 kati ya zaidi ya 10,000 wanaofadhiliwa na Serikali.
Lakini, alisema tayari amezungumza na
Bodi ya Mikopo ambayo imemwahidi kuleta fedha hizo haraka, na kuwaomba
wanafunzi kurejea madarasani kuendelea na masomo.
MTANZANIA
Baadhi ya wabunge wamezungumzia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wakisema ufisadi unaoendelea nchini ni matokeo ya kupuuzwa kwa ripoti za mkaguzi huyo.
Maoni ya wabunge hao yametolewa baada ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuibua ufisadi
mkubwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na
Serikali Kuu kwa ukaguzi ulioishia Juni mwaka jana.
Wabunge wengi wamesikitishwa na kitendo
cha Serikali kufumbia macho ripoti hizo huku wengine wakisema
wabadhirifu wote serikalini ni wezi wanaostahili kushtakiwa na
kufilisiwa.
Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Baruwani
(CUF), alisema kwa mfumo wa sasa ni vigumu ubadhirifu wa fedha za
Serikali kukomeshwa kwa vile ni watendaji wanaotakiwa kusimamia ripoti
hiyo ndiyo wanaohusika na wizi huo.
“Kesi ya mbuzi huwezi kumpelekea fisi,
ninachokiona mimi hapa inabidi CAG apewe meno maana kwa sheria ilivyo
CAG akikagua anaishia kutoa ripoti tu baada ya hapo kazi ni ya watu
wengine.
“Tumeona udhaifu huo, sisi kama Bunge
inabidi tuishauri Serikali ilete sheria tuifanyie mabadiliko CAG
aongezewe meno haya mambo yatakwisha,” alisema.
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer
(CCM), aliitaka Serikali kufungua macho juu ya ripoti za CAG na kueleza
kuwa bila hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watendaji wabadhirifu fedha
nyingi zitaendelea kupotea.
“Hawa
watendaji wanaoisababishia Serikali hasara inabidi washitakiwe na
wafilisiwe. Mgonjwa bila dawa hawezi kupona lakini pia mwizi bila
kukamatwa na kuadhibiwa hawezi kuacha kuiba,” alisema.
Alisema inasikitisha kuona kila mwaka
mkaguzi huyo anaendelea kufanya ukaguzi na kubaini uchafu lakini hakuna
hatua zozote zinazochukuliwa. “Fedha hizi ni sawa na bajeti nzima ya wizara moja lakini zinapotea,” alisema.
Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina
(CCM), alisema ubadhirifu wa aina hiyo hauwezi kumalizika iwapo rais wa
nchi hatakua mkali kupambana na ubadhirifu.
Ntukamazina anayejulikana kama senior
citizen (raia mkongwe), alisema CAG hawezi kuongezewe meno zaidi ya hapo
na kwamba kinachotakiwa ni mamlaka ya nchi kulitambua hilo na
kulisimamia.
“Utekelezaji wa ripoti hizi ni suala la
leadership (uongozi), huwezi kupambana na ufisadi kama wewe si msafi.
Katika hili Serikali inabidi ichukue hatua, tunaposema Serikali ni rais,
yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuajiri na kuwafukuza hawa watendaji.
“Mchezo huu wa kulindana hatufiki mbali.
Mimi siku zote nimekuwa nikikosoa ninapoona Serikali inakosea na baadhi
ya mawaziri wamekuwa wakinichukia, lakini nasema rais anatakiwa awe
serious (dhamira ya dhati) na hizi ripoti za CAG,” alisema.
No comments:
Post a Comment