07 May, 2015

Kama ulikosa habari zilizokua magazetini leo MAY 7 hizi hapa zipitie

late
HABARILEO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imejikuta kwenye wakati mgumu baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kubaini kiasi cha Sh milioni 96.6 kimetumika kubomoa jengo bovu mali ya ofisi hiyo, ili kupisha ujenzi wa ofisi mpya za mkuu wa mkoa huo.

Hayo yalibainika jana jijini Dar es Salaam, mbele ya Kamati hiyo wakati Ofisi hiyo ikipitia ripoti ya ukaguzi wa hesabu kutoka kwa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Wakati kamati hiyo ikifanya mapitia hayo, CAG alibaini matumizi makubwa ya fedha zilizotumika kwa ajili ya kubomoa jengo bovu, lililoko jirani na ofisi za Wilaya ya Temeke ili kupisha ujenzi wa jengo la Mkuu wa Mkoa huo, kutokana na ofisi hizo kwa sasa kuwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara eneo la Ilala.
Akihoji matumizi ya fedha hizo, mjumbe wa kamati hiyo, Modestus Kilufi alimuomba mwenyekiti wa kamati hiyo kwa jana Gaudence Kayombo kumwagiza CAG, kupitia hesabu hizo, ili kubaini matumizi yake, kwani ni fedha nyingi zilizotumika kwenye kazi hiyo.
“Tunamuomba CAG atuthibitishie matumizi ya fedha hizo, hiki ni kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kwenye kazi hiyo, ni vyema wakaangalia kazi iliyofanywa kama ina thamani na fedha iliyotolewa na tunaomba majibu yatufikie kabla ya Mei 15, mwaka huu”.
Wakijitetea mbele ya kamati hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Terezia Mmbando, Mhasibu Mkuu wa Mkoa, Shaban Mhando, na maafisa wengine walioambatana na viongozi hao wa mkoa, walishindwa kutoa majibu yenye ushawishi kwa kamati hiyo kukubaliana na matumizi ya fedha hizo.
Tuliomba hazina shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kujenga jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini tulipewa shilingi milioni 150 tu, tulikuwa kwenye kipindi kigumu cha hasa ukizingatia jengo la mkuu wa mkoa la sasa lipo kwenye hifadhi ya barabara”,  Mmbando.
HABARILEO
Wakili mwandamizi wa kujitegemea wa jijini hapa, Manase Keenja mkazi wa Kijenge Mwanama, Arusha, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za serikali na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh milioni 320.
Keenja anayemiliki kampuni ya uwakili ya Keenja Advocates iliyopo mtaa wa Azimio jijini Arusha alitiwa mbaroni Mei Mosi mwaka huu majira ya saa 6 mchana kwa tuhuma hizo za kughushi.
Wakili huyo mkongwe mbali ya kujipatia fedha kwa njia hiyo, pia amekamatwa na mihuri mbalimbali ya serikali, ikiwemo ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini, mhuri wa ofisi ya Ardhi Halmashauri ya Jiji la Arusha na mihuri ya Mahakama zote za Mkoa, Wilaya na mwanzo za Mkoa wa Arusha.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Edward Balele alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa wakili huyo na mwandishi wa gazeti hili alikiri na kusema kuwa polisi bado inamshikilia kutokana na upelelezi kutokamilika na upelelezi ukikamilika atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Balele alisema polisi haiwezi kumwachia kwa sasa mpaka upelelezi utakapokamilika, kwani kuachiwa haraka kunaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.
Alisema kukamatwa kwa wakili Keenja kumetokana na malalamiko ya wafanyabiashara watatu tofauti wa Jiji la Arusha walioripoti kituo kikuu cha polisi Arusha juu ya ‘kutapeliwa’ mamilioni ya shilingi na wakili huyo.
Kamanda huyo alisema miongoni mwa wafanyabiashara wanaodaiwa kudhulumiwa na wakili huyo ni pamoja na Macklin Temu anayemiliki kampuni ya maduka ya vipuri vya magari ya Denso, ambaye inaelezwa amepoteza Sh milioni 120 mbele ya wakili huyo.
Inadaiwa alichukuliwa fedha hizo Aprili 23 mwaka 2013 kwa kuuziwa kiwanja namba 12 kilichopo katikati ya Jiji la Arusha ambacho kinamilikiwa na mtanzania mwenye asili ya kiasia Ragieder Kumar, ambaye kwa sasa ni marehemu kwa kiasi hicho cha fedha.
MWANANCHI
Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameunda kamati kwa ajili ya kushughulikia mgomo wa madereva uliotikisa nchi kwa siku mbili, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema haoni mantiki ya kuunda tume kuchunguza jambo ambalo linafahamika.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni makatibu wakuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kazi na Ajira na Wizara ya Uchukuzi.
Wengine ni wajumbe watatu kutoka Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) na wajumbe watatu kutoka Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), mjumbe mmoja kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani na mmoja Sumatra.
Pia wanaingia wajumbe wengine watano ambao wanawakilisha madereva baada ya mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kukubaliana na viongozi wao juzi.
Lakini Nape haoni kama kulikuwa na haja ya kuunda kamati ya kushughulikia tatizo ambalo linajulikana.
“Kama huundwa kuchunguza mambo ambayo hayafahamiki, lakini madai ya madereva hao yanafahamika,” alisema msemaji huyo wa chama tawala alipotakiwa kuzungumzia maoni ya baadhi ya wananchi kwamba mgomo huo ni matokeo ya CCM kushindwa kuwajibika na hivyo kutostahili kuendelea kupewa nafasi ya kuongoza nchi.
“Watupe au watunyime kura, ni kweli CCM na Serikali yake inapaswa kutatua suala hilo. Ndiyo maana mimi nasema sikubaliani na tume. Serikali ishughulikie suala hili kwa kuwa madai ya madereva hao yanafahamika,”  Nape.
“Mimi sioni mantiki ya kuunda tume kwa tatizo ambalo linajieleza. Madai ya madereva na wamiliki wa magari yanajulikana, tume ya nini? .
Madereva waliendesha mgomo huo nchi nzima wakipinga uamuzi wa serikali kuweka sharti jipya la kwenda kupata mafunzo ya muda mfupi kabla ya kupewa leseni upya na kutaka Serikali iwalazimishe waajiri wao kuwapa mikataba inayozingatia maslahi yao.
Wakati Nape akisema hayo, CCM mkoani Mbeya imeilaumu Serikali kwa kuchelewesha mazungumzo na madereva na hatimaye kusababisha mgomo huo kuwaathiri wananchi bila sababu za msingi.
MWANANCHI
Chifu wa Wazanaki, Joseph Wanzagi amasema CCM haitakiwi kuvibeza vyama vya upinzani hasa baada ya kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), huku akisema atakuwa mtu wa kwanza kumshauri Makongoro Nyerere kugombea urais wakati ukifika.
Kiongozi huyo wa kimila alisema hivi sasa Ukawa ina nguvu kubwa tofauti na wakati vyama hivyo vilipokuwa havijaungana na kutaka pande zote mbili kuheshimiana licha ya tofauti zao za kiitikadi.
Hata mimi naamini kuwa mgombea atakayeteuliwa na CCM ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuwa Rais, lakini Chama cha Mapinduzi kisibeze wapinzani, hasa baada ya kuungana na kuanzisha Ukawa,” alisema Chifu Wanzagi alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa chama hicho tawala kinapoteua mgombea ni kama kimemtangaza Rais wa Tanzania.
Vyama vinavyounda Ukawa- Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD- vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kwenye nafasi ya urais hadi udiwani na tayari umoja wao ulifanya kazi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambako vyama hivyo vilitwaa viti kwenye maeneo mengi ambayo CCM ilikuwa inayashikilia.
Kiongozi huyo ambaye anatoka kwenye ukoo wa Nyerere alisema si mkereketwa sana wa masuala ya kisiasa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa ushindani wa kisiasa lakini anaamini CCM itashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Alisema anakubaliana na msimamo wa Mwalimu Nyerere kwamba CCM ikisimamisha mgombea wa urais, ndiye anakuwa rais na anaamini mgombea atakayepitishwa na chama hicho kikongwe atashinda.
Kuhusu Makongoro, aliyemtaja kuwa ndiye mhimili wa familia ya Nyerere kisiasa, Chifu Wanzagi alisema: “Kwenye familia ya Nyerere, hakuna mwanasiasa mzuri zaidi ya Makongoro na kama hatoshi kwa nafasi hiyo, basi familia ya Mwalimu haina mwanasiasa tena.
MTANZANIA
Askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaolinda amani katika Kikosi cha Umoja wa Mataifa (MONUSC) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameuawa na waasi.
Askari hao ambao majina yao hayajatambuliwa, waliuawa juzi alasiri katika shambulio la kushtukiza mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia msemaji wa MONUSCO, Kanali Felix Basse, ilisema mbali ya waliouawa, wanajeshi wengine 13 walijeruhiwa na wanne hawajulikani waliko.
Shambulio hilo lilitokea wakati wanajeshi hao wakiwa katika doria ya kawaida katika Kijiji cha Kisiki, ambako vikosi vya Serikali ya DRC vinapambana na waasi wa Uganda wenye itikadi kali ya Kiislamu – ADF.
Kijiji hicho kipo umbali wa kilomita 50 kaskazini mwa mji wa Beni katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini.
Taarifa zinasema askari hao walipofika katika kijiji hicho walikuta waasi wamejificha pande mbili za barabara.
Kutokana na hali hiyo, walijikuta wakishambuliwa kwa silaha nzito kutoka kila upande jambo ambalo liliwapa wakati mgumu kujibu mashambulizi.
Mmoja wa watu walihojiwa alisema: “Waasi walinipiga risasi wakanivunja mguu, mimi ni dereva teksi… sababu kubwa ya kufanya mashambulizi haya wanadai kiongozi wao kakamatwa na Tanzania.
“Walikuwa wamefunga eneo lote la barabara, wana silaha nzito… sijui hata abiria niliokuwa nao wako hai ama la,” alisema mtu huyo.
Juzi, jeshi la DRC lilisema limewaua wapiganaji 16 wa ADF wakati wa mapambano makali katika eneo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Shambulizi hilo ni la pili dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN) ndani ya saa 48, baada ya helikopta ya MONUSCO kushambuliwa na watu wasiojulikana siku ya Jumatatu.
Mkuu wa operesheni za MONUSCO, Martin Kobler, alilaani shambulio hilo dhidi ya kikosi cha wanajeshi wa Tanzania kinacholinda amani katika kijiji hicho.
MTANZANIA
Kamati ya Ukweli na Maridhiano ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), imetangaza kumvua uanachama Mwenyekiti wa chama hicho, Agustino Mrema.
 Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Joram Kinanda alisema kuwa kamati hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia kwa kina malalamiko yaliyokuwa yakimuhusu Mrema, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa mbali na Mrema wengine waliovuliwa uanachama ni Hamisi Mkadamu, Antoni Mapunda, Nancy Mrikaria, Dominata Rwechungura, Maxmilian Lymo, Richad Lyimo, Hamisi Mkumba na Stanley Temba.
Kinanda alisema kuwa maazimio hayo yamepelekwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa taratibu za kisheria pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa upande wake Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, alipotafutwa ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema kamati hiyo haitambuliki kisheria.
Kamati hiyo haitambuliki kisheria, na hata Mrema mwenyewe amekuwa akipinga TLP kuwa na kamati ya aina hiyo na hata viongozi wake hawatambuliki, ” alisema
MTANZANIA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba amesema Jamhuri inasema uongo kwamba Jeshi la Polisi liliwanyima kibali cha kuandamana na kwamba akiwa na msafara wa magari alifuatana na wafuasi wake kuelekea Mbagala Zakhem.
Profesa Lipumba anadai si kweli kwamba walifanya maandamano, ispokuwa walipigwa tu wao na wala hawakukamatwa wakiwa katika maandamano.
Alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati mshtakiwa huyo na wenzake 31 walipokuwa wakisomewa maelezo ya awali ya kesi inayowakabili.
Si kweli kwamba tulifanya maandamano, tulipigwa tu hatukuandamana sisi, wala hatukukamatwa katika maandamano,” Lipumba.
Kwa kuongozwa na wakili wa utetezi, Twaha Taslima, walikana Januari 26, mwaka huu kunyimwa kibali cha kufanya maandamano kwa sababu hawakuwahi kuomba kibali, walitoa taarifa ya kufanya maandamano.
Si sahihi kusema Polisi iliwanyima kibali, hapakuwa na maombi ya kibali, CUF walitoa taarifa ya kufanya maandamano,Taslima.
Pia Profesa Lipumba na washtakiwa wengine walikana kusikia Polisi wakitoa onyo katika maeneo ya ofisi za chama hicho wilayani Temeke wakiwataarifu waandamanaji kutawanyika kwani mkusanyiko haukuwa halali.
NIPASHE
Ni dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingiwa hofu inayokifanya kishindwe kutangaza mchakato na ratiba za vikao vya uteuzi wa wagombea wake wakiwamo wa urais na ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Kufikiwa kwa hatua kama hiyo kwa vyama vikubwa vya upinzani nchini, kunaifanya CCM ibaki njia panda, hali iliyo tofauti na nyakati kama hizi katika kuelekea chaguzi zilizofanyika hususani zikihusisha vyama vingi tangu kuanzia 1995.
Taarifa za uhakika zilizothibitishwa na vyanzo tofauti ndani ya CCM zilieleza kuwa, hali ilivyo mwaka huu kwa chama hicho inachangiwa na sababu tofauti, ikiwamo mkakati wa `kuwatosa’ wagombea wasiokubalika kwa baadhi ya viongozi na `kuwabeba’ wasiokuwa na mvuto kwa wapiga kura.
“Hali hii inawafanya (viongozi) washindwe kutimiza wajibu wao katika kutoa ratiba na kutangaza mchakato wenye kutoa taarifa na uhuru kwa wanachama wake kuchukua fomu za uteuzi,” kilieleza chanzo chetu.
Tangu mwaka 1995, CCM imekuwa ikitangaza mchakato na ratiba za kura za maoni na kuwapata wagombea kabla ya vyama vya upinzani, hali iliyovifanya  vyama vya upinzani kutoa fursa kwa baadhi ya walioshindwa katika kura za maoni (za CCM) kugombea nafasi tofauti kupitia vyama hivyo.
Wakati CCM ikiendelea kuwa kimya kuhusu mchakato na ratiba ya kura za maoni kuwapata wagombea wake, hatma ya adhabu ya makada sita waliokuwa wakichunguzwa kwa tuhuma za kufanya kampeni zenye mwelekeo wa kukigawa chama, haijajulikana.
Makada hao walipewa adhabu ya kuchunguzwa mienendo yao kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kimahesabu, adhabu hizo zilipaswa kufikia ukomo wake Februari 18, mwaka huu.
“Kwa chama kikongwe kama CCM kushindwa kusema kama adhabu ya miezi 12 imekwisha au la, ni ishara ya kutokuwapo uthubutu na dalili za hofu inayokiangamiza chama hicho,” alieleza mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa.
Hata hivyo, Ofisa mmoja katika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam, alisema kuchelewa kwa mchakato na ratiba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa utendaji kazi ndani ya CCM.
NIPASHE
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, imezindua program ya uimarishaji ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa kutumia mbwa maalum kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Wizara za Uchukuzi, Mambo ya Ndani na Maliasili na Utalii, ndizo zitakazohusika na program hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema jijini Dar es Salaam juzi  kuwa program hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Chini ya mpango huo, Polisi wa Tanzania watapatiwa mafunzo nchini Marekani ya kutumia mbwa maalum katika maeneo hayo ifikapo Septemba, mwaka huu.
Waziri Nyalandu alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi wa namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa lao.
Kamishina wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, Gil Kerlikowske, kwa upande wake alisema baada ya kupatiwa mafunzo katika vyuo vya idara hiyo, Polisi wa Tanzania watarejea nchini wakiwa na mbwa hao tayari kwa kuanza kazi ya kupambana na wasafirishaji haramu wa dawa za kulevya na bidhaa zitokanazo na wanyamapori.
“Program za kutumia mbwa hawa maalum, huongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa bandari na viwanja vya ndege kubaini bidhaa haramu zinazoingizwa au kutolewa nchini,”.
Ni mara ya kwanza katika historia ya idara hiyo kuwezesha matumizi ya mbwa katika kubaini pembe za ndovu.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Miundombinu katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Aloyce Matei, alisema suala la ulinzi na usalama, ni kati ya vipaumbele vikubwa vya mamlaka hiyo.
“Tunakaribisha sana program hii katika bandari yetu,” alisema Matei aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA, Awadh Massawe.
Baada ya mafunzo hayo, wataletwa mbwa maalum wanne nchini; wawili Bandari ya Dar es Salaam na wengine idadi kama hiyo Uwanja wa Ndege.
NIPASHE
Jiji la Dar es Salaam limetikiswa na matukio ya uhalifu unaofanywa na magenge ya vijana kuvamia majumba ya watu, maduka na sehemu nyingine za biashara na kupora fedha na vifaa mbalimbali hasa vya elekroniki.
Magenge hayo ya wahalifu hutenda uhalifu wakiwa katika makundi ya watu watano hadi 20 wakiwa na silaha mbalimbali zikiwamo za moto.
Juzi kundi la watu 20 wanaodhaniwa kuwa  majambazi lilivamia nyumba ya mapadri wa Kanisa Katoliki na kupora fedha na mali nyingine.
Majambazi hao walivamia Parokia ya Kilungule, wilayani Temeke na kupora fedha taslimu na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni nne.
 Paroko Msaidizi wa parokia hiyo, Padri Pascal Libongi, alisema majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia jana, waliamshwa na walinzi wa nyumba hiyo kuwa kuna kundi la vijana wenye silaha wanavamia ndipo walipotoka na kujificha.
“Tuliamshwa na mlinzi wa ndani kuwa tunavamiwa ndipo tukajificha, nilijificha bafuni na Paroko alijificha kwingine, walifika wakapanda kwenye geti na kufungua mlango kwa ndani na kuingia kisha wakavunja mlango mkuu kwa baruti,” alisema.
Alisema watu hao waliingia ndani ya geti huku wakipiga kelele wakisema wanataka kuua na kwamba walitumia muda wa dakika 10 hadi 15 kuvunja mlango kwa kutumia silaha walizokuwa nazo na walifyatua baruti.
Baada ya kuingia ndani walizima umeme kwenye main switch, wakabishana kwa muda, waliambizana twende kwenye chumba cha bosi, waliingia wakachukua walichoweza na walitoka sebuleni na kuchukua seti ya TV nchi 24 na kuondoka,Libongi.
Padri Libongi alisema ndani ya chumba cha Paroko walichukua simu tatu na fedha taslimu Sh. milioni 3.2 na TV na baadaye waliondoka huku wakipiga kelele.

Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO,SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>Zawadi_mawere. Youtube>>>MAWERE TV.


No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...