09 May, 2015

Hatima ya Lowassa, Membe sasa Mei 20

Filimbi ya kuanzisha mbio za urais kwa tiketi ya CCM itapulizwa Mei 23 baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala, huku makada sita walio ‘kifungoni’ wakitarajia kujua hatima yao kwenye mbio hizo Mei 20. 

 

CCM imekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa uchaguzi, unaohusisha ratiba ya chama hicho, kupitishwa kwa Ilani ya Uchaguzi na taratibu nyingine za kugombea uongozi, kiasi cha kutia wasiwasi baadhi ya wanachama wake, wakiwamo makada sita ambao walifungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujihusisha na kuwania madaraka baada ya kubainika kukiuka taratibu.
 

Makada hao waliopewa adhabu na Kamati Kuu ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
 

Wengine Steven waziri, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula, January Kamamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na William Ngeleja, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
 

Mbali na makada hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba aliwahi kupewa barua ya katazo la kufanya ziara na mikutano ya kibinafsi yenye viashiria vya kampeni za urais.
 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuthibitisha kuwapo kwa vikao vya vyombo hivyo viwili wiki mbili zijazo.
 

“Kwanza habari hizo siyo za kweli, nazisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwako,” alisema Nape alipoulizwa kuhusu tarehe za vikao hivyo.
 

“Kwanza umeshaandika stori yenu halafu ndiyo mnanipigia kuthibitisha. Inakuwaje msemaji wa chama hana habari, halafu nyinyi Mwananchi muwe nazo?” alihoji Nape.
 

Hata hivyo, habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20, kuandaa taratibu zote za uchaguzi na siku inayofuata, yaani Mei 21 iwasilishe kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokuwa cha siku mbili.
 

Habari hizo zinaeleza kuwa vikao hivyo viwili vinatarajiwa kutoa ratiba na utaratibu wa kuchukua na kurudisha fomu kwa waombaji wa nafasi za udiwani, ubunge na urais na kupokea na kupitisha ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
 

Chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM kimelieleza Mwananchi  kuwa vikao hivyo vitahitimisha suala la wagombea sita wa urais waliopewa onyo kali kwa kuanza kampeni mapema na kushiriki vitendo vya utovu wa nidhamu.
 

Habari kutoka ndani ya CCM pia zinaeleza kuwa katika eneo la mchakato ripoti za Kamati Ndogo ya Maadili, chini ya makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula itatikisa vikao hivyo hasa uchunguzi wake kuhusu mienendo na harakati za kuwania urais.



Wasiwasi na shauku ya ripoti ya kamati hiyo inatokana na kauli za hivi karibuni za Mangula kuwa chama hicho kinazo taarifa za makundi ya makada wanaosaka urais na matumizi makubwa ya fedha.
 

Makada hao, ambao miongoni mwao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye mbio za urais, walidaiwa kukiuka taratibu inayozuia wanachama kuanza kampeni mapema na adhabu yao ilitakiwa imalizike Februari mwaka huu, lakini ikaongezwa kwa maelezo kuwa Kamati ya Maadili bado inaendelea na uchunguzi.
 

Mbali na makada hao sita, wengine wanaotajwa kuwa na nia ya kuchukua fomu ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ambao jana walitangazwa kusafishwa dhidi ya tuhuma za kutowajibika katika Operesheni Tokomeza.
 
 Wawili hao walilazimika kuachia ngazi mapema mwaka jana baada ya Kamati ya Bunge kutoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwamo kwenye operesheni hiyo iliyolenga kupambana na ujangili.
 

Vilevile, vikao hivyo vinatarajiwa kupokea na kujadili mapendekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2015-2020.
 

Vyanzo vingine vya habari vimeeleza kuwapo pia kwa ajenda ya hali ya siasa inayohusishwa na misuguano ndani ya chama bara na visiwani, uandikishaji wapigakura, mchakato wa Katiba mpya na jinsi ya kupambana na wapinzani, hasa Ukawa.
 

Kamati Kuu inatarajia kutumia vikao hivyo kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika kwa wananchi kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha urais, wabunge na madiwani. Chanzo: Mwananchi 

Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO,SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>Zawadi_mawere. Youtube>>>MAWERE TV.

TUPATIE MAONI YAKO HAPA 

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...