HABARILEO
Wakati ajali za barabarani zikiendelea
kumaliza nguvu kazi ya Taifa na kuumiza vichwa vya Watanzania kuhusu
suluhisho la ajali hizo, imefahamika moja ya tatizo sugu ni kukosekana
kwa madereva wenye taaluma stahiki, ingawa wana leseni.
Wiki hii peke yake, ajali tatu za mabasi
zilizotokea Mbeya, Morogoro na maeneo ya Mwanza, zimesababisha vifo vya
watu 40 ndani ya siku sita.
Tayari Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
ametoa takwimu za vifo vilivyotokana na ajali za barabarani kati ya
Januari Mosi mwaka huu hadi Aprili 12, sawa na siku 102 vifo 969.
Kwa upande wa usafiri wa kutumia pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda),
Kamanda Mpinga ameeleza kuwa kati ya Januari na Machi, sawa na siku 90
madereva wa bodaboda ambao Serikali ilishakiri kuwa wengi hawana leseni,
wamesababisha vifo vya watu 220.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii,
mmoja wa wataalamu wa mambo ya usafirishaji nchini, alisema mabasi ya
kusafirisha abiria nchini, ni mengi kuliko idadi ya madereva wenye
taaluma ya kuendesha abiria.
Mazingira hayo ni sawa na usafiri wa
bodaboda, ambao nao unakabiliwa na tatizo kubwa na pikipiki nyingi
zilizosajiliwa, kuliko idadi ya madereva wake waliopatiwa leseni.
“Mimi
nina uhakika kabisa ajali hizi zina uhusiano mkubwa na mafunzo kwa
madereva, kwa kuwa kama dereva angekuwa anapona katika ajali, tungesema
amepata mafunzo stahiki, lakini wengi wanakufa kwakuwa hawana mbinu za
kupambana na ajali,” alisema.
Alisema ni dhahiri kuwa madereva wa
Tanzania hawana ujuzi wa kutumia vyombo hivyo na kufafanua kuwa, vyombo
wanavyoendesha vinajulika vinaua, ndio maana katika mafunzo madereva
lazima wapewe mbinu ya kujilinda kama inavyofanyika katika nchi
nyingine.
Mtaalamu huyo alihoji iweje marubani wa
ndege binafsi, zinazobeba abiria wanne hadi sita, wapelekwe katika
mafunzo kila baada ya miaka minne, lakini kwa madereva wanaobeba abiria
zaidi ya 65, wanakataa kupelekwa mafunzo baada ya miaka mitatu na
kuongeza kuwa hapo kuna tatizo lazima liangaliwe.
Alisema madereva wanapaswa kuelimishwa
kuwa mafunzo hayo, ndio mwanzo wa kuandaa kanuni za mafunzo kwa
madereva, ili watambulike rasmi kama walivyo marubani na manahodha.
Uzoefu nchi nyingine Mtaalamu huyo
alisema duniani kote udereva hususan wa abiria, ni kada ya juu
inayolipwa mshahara mkubwa, huku mafunzo yake yakiwa magumu na huchukua
muda mrefu.
Alitoa mfano wa nchi ya Uingereza,
ambako mtihani hufanyika kwa kutumia mtandao wa kompyuta, ambapo kama
dereva mtarajiwa akifaulu kwa kupata zaidi la asilimia 70, cheti
kinajiprinti chenyewe.
Alisema katika mafunzo hayo, hakuna
kujuana bali kompyuta tu zinafanya kazi na hivyo ufaulu wake na kupata
cheti au leseni ni halali, kuliko kufanya mtihani kwa kujuana na kupeana
leseni.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mitihani
hiyo katika baadhi ya nchi ikiwemo Afrika Kusini na Japan, hata leseni
ya gari dogo, dereva lazima afanye mtihani kabla ya kupata leseni.
HABARILEO
Serikali imerejesha mafunzo ya madereva
kila baada ya miaka mitatu wakati wa kumalizika kwa muda wa leseni zao,
huku ikifafanua kuwa elimu watakayoipata ina umuhimu katika kazi zao,
kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sekta hiyo.
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro
Mahanga, alitangaza uamuzi huo wa Serikali jana katika mkutano kati
yake na viongozi wa madereva wa mabasi nchini.
Mkutano huo umefanyika kama
ilivyoahidiwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, wakati
alipokuwa akijitahidi kumaliza mgomo wa madereva uliofanyika Aprili 10
mwaka huu, wakati walipokuwa wakipinga pamoja na mambo mengine, sharti
la kwenda shule ili kupata leseni mpya.
Madereva hao walitaka Serikali ifanyie
marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani, kwa kuondoa kipengele
kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa
mafunzo ya muda mfupi kila wakati leseni zao zinapoisha, ili kupata sifa
ya kupata leseni nyingine.
Sababu ya kupinga kupata mafunzo,
ilidaiwa kuwa utaratibu huo uliotangazwa Machi 30, mwaka huu,
ulianzishwa bila kushirikisha madereva katika kuuandaa.
Pia walipinga kutakiwa kujilipia gharama
za shule hiyo ambazo walidai ni Sh 560,000 kwa magari ya kawaida na Sh
200,000 kwa magari ya abiria.
Sababu nyingine iliyochangia wapinge
shule hiyo, walidai ni kukosekana kwa mikataba ya ajira, inayoweza
kuwahakikishia kulindwa kwa kazi zao hadi wanapomaliza mafunzo.
Madai mengine yaliyokuwa nje ya shule
hiyo, madereva hao walitaka kuondolewa kwa faini ya Sh 300,000 kwa kila
kosa la barabarani na kuitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini
na Nchikavu (Sumatra), kuhakiki uhalisia wa dereva anayeandikishwa na
mmiliki wa chombo husika.
Majibu ya Serikali Mahanga aliyekuwa
Mwenyekiti wa kikao hicho, alisoma tamko la Serikali lililoeleza kuwa
pamoja na kurejesha mafunzo hayo, utekelezaji wake hautafanyika mara
moja kwa kuwa Kanuni zake hazijakamilika.
“Tangazo hili (la kwenda shule)
limetolewa kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo kazini kwa wafanyakazi na
madereva kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine,” alisema Mahanga.
Alisisitiza kuwa baada ya miaka mitatu
ya leseni, dereva atatakiwa kupata mafunzo mafupi, ambayo ni kati ya
siku tatu hadi saba na atakayegharimia mafunzo hayo ni mwajiri, si
mfanyakazi na ni katika chuo chochote kinachotambulika.
Akifafanua, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Ndani, Mwamini Malemi aliyekuwepo katika mkutano huo, alisema
mitaala ya mafunzo hayo bado inaandaliwa, hivyo si rahisi Kanuni hiyo
kuanza kutekelezwa mwaka huu hata kama zitakamilika.
Kuhusu mikataba ya ajira ambayo
ililalamikiwa mno na madereva wakati wa mgomo, Mahanga alisema Serikali
itapitia upya mikataba hiyo ili kuhakikisha mambo yote muhimu
yanazingatiwa.
Akiongezea hoja katika suala la
mikataba, Malemi alisema ni lazima mikataba iwe imekamilika kabla ya
kuanza kutumika kwa kanuni ya kwenda shule, ili ioneshe wajibu wa
mwajiri katika kumsomesha mfanyakazi.
Kuhusu kauli iliyotolewa na Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ya kuondoa tochi za
kupima mwendo kasi barabarani, Mahanga alisema matumizi ya tochi
zinazotumika kupima mwendo kasi na ratiba ni sehemu ya utekelezaji wa
Sheria za Usalama Barabarani.
MTANZANIA
Raia wa Tanzania wanaoishi Afrika Kusini
sasa wanadaiwa kushika silaha tayari kwa mapambo dhidi ya vikundi vya
raia wa Taifa hilo vinavyoshambulia wahamiaji wa Kiafrika.
Taarifa zilizolifikia Gazeti hilo kutoka
kwa Watanzania hao imeeleza hatua hiyo imefikiwa baada ya kupatikana
kwa taarifa zinazodai kuwa wenzao wawili wameuawa katika machafuko ya
jiji la Durban ambayo chanzo chake ni mashambulizi yanayofanywa na raia
wan chi hiyo dhidi ya wageni.
Mmoja wa Watanzania anayeishi Cape Town Pius Mbawala
alieleza kuwa taarifa za mauaji ya wenzao zimewasikitisha sana na
kwamba hadi sasa hakuna kiongozi yoyote wa ubalozi wa Tanzania
aliyewasiliama nao ili kujua hali za usalama wao tofauti na balozi za
nchi nyingine.
Mbalawa alisema kwa muda mrefu sasa
maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini humo wamekuwa na uhusiano wenye
shaka na Watanzania walioko huko tofauti na wanavyopaswa kujua ukazi wao
kwenye Taifa hilo.
Alisema Raia wa Tanzania wanaoishi
nchini humo wamejiunga katika makundi madogo madogo kulingana na maeneo
wanayoishi kwa ajili ya kujilinda wenyewe na kila kundi hivi sasa
limejihami kwa silaha.
MTANZANIA
Umoja wa madereva nchini umesema
umemwandikia barua Waziri mkuu Mizengo Pinda kulalamikia hatua ya
Serikali kutoyashughulikia madai yao.
Pia kama hali hiyo itaendelea hivyo wametishia kugoma tena kufanya mgomo mwingine.
Katibu wa Umoja huo Abdallah Lubala
alisema kilichofanyika walipokutana na na Naibu Waziri wa Kazi na ajira
Dk.Makongoro Mahanga ni siasa.
“Serikali
inatufanyia siasa kwa kuwa tulipofika badala ya kukutana na Waziri ili
kujadili suala letu tuliishia kusomewa barua na Mahanga inayonukuu kikao
cha April 9 tulipokutana na Waziri, sasa hapo tunajiuliza kama walikuwa
na majibu kama haya kwa nini walishindwa kuyasoma?” Lubala.
Alisema juzi ikiwa ni siku moja baada ya
kukutana na Mahanga kilifanyika kikao na wamiliki wa magari
kilichozidisha shaka yao kwa kuwa hawana imani nacho kutokana na wao
ndio waliomba mkutano huo.
Katika barua hiyo ambayo ina kichwa cha
hbabari kuhusu tamko la Serikali juu ya hoja za madereva zilizotolewa
katika kikao kati ya waziri wa kazi Kabaka na viongozi hao,Serikali
ilisema itachukua hatua ikiwemo ya kupitia upya mikataba ya ajira zao
ili kuhakikisha mambo muhimu kama mishahara,malipo ya saa za
ziada,likizo na michango ya hifadhi yanatekelezwa.
MWANANCHI
Mmoja wa majeruhi wa ajali iliyoua watu
19, Mariam Manfredy (28) aliyevunjika mguu wa kushoto, anasimulia ajali
hiyo na kusema chanzo ni mwendo kasi na kuungua kwa breki.
Gari hilo lilikuwa ‘limeshona’ abiria,
lilikuwa likitoka jijini Mbeya kwenda Kiwira wilayani Rungwe kabla ya
kuanguka eneo la Mto Kiwira na kuua watu 18 palepale na mmoja alifia
Hospitali ya Igogwe huku wengine watatu wakijeruhiwa.
Mariam aliyelazwa katika Hospitali ya
Rufaa Mbeya (MRH), alisema alipanda basi hilo katika Kijiji cha Simambwe
akienda Kiwira kununua bidhaa za biashara.
“Tulipofika Kijiji cha Ndaga,
magurudumu yalianza kutoa cheche na moshi jambo lililomfanya kondakta
kuteremka na kuzima kwa maji na kwamba wengi walisema breki zimeungua
kwa kuwa kulikuwa na harufu kali ya kitu kinachoungua.
“Baada ya kuzima moto kwenye matairi
hayo, dereva aliendelea na safari kwa kasi na ndipo basi lilipoongeza
kasi kubwa ambayo iliwafanya abiria wote wapige kelele kumtaka dereva
apunguze mwendo, lakini yeye hakusema lolote.
“Mimi nilikuwa nimesimama mlangoni na
kondakta wa gari hilo na hata ajali hiyo ilipotokea sikuiona bali
alijikuta nikiwa kwenye maji hadi nilipookolewa na wasamaria wema.
“Nilipotokea ni kama Mungu tu hakutaka
nife…gari ilipinduka vibaya na wengi wamekufa, jamaa zangu na wengi
tulikuwa tunakwenda kununua bidhaa kwa ajili ya biashara zetu.”
Katika ajali hiyo watu 19 walipoteza maisha na hadi jana maiti 15 kati ya 18 zikichukuliwa na ndugu zao.
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ilifurika
umati wa watu waliokuja kushuhudia na kutambua majeruhi pamoja na
kuchukua miili ya jamaa zao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo,
Aminiel Ngamuo alisema baada ya ajali ndugu wa marehemu walimimika juzi
jioni kuzitambua na walifanikiwa kuwatambua ndugu zao huku maiti tatu
za wanaume zikiwa zimebaki hadi jana mchana.
Hata hivyo Dk Ngamuo alishindwa kutaja majina ya waliotambuliwa akisema majina yalifungiwa kwenye ofisi zingine.
Maeneo mengi ya mkoa wa Mbeya yalikuwa
na vilio hasa katika maeneo ya Iyunga, Nzowe, Uyole na Mwanjelwa ambako
abiria hao walitokea.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema
anasubiri kukamilika kwa utaratibu wa CCM wa kugombea urais ili aingie
rasmi kwenye mbio hizo kwa kuwa anaridhika na mambo matatu ambayo
anasema yanamfanya ashawishike kugombea nafasi hiyo ya juu katika siasa
nchini.
Sitta, mwanasiasa mkongwe na Spika wa
Bunge la Tisa, ni mmoja kati ya makada wa chama hicho tawala
wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais
kumrithi Jakaya Kikwete, ambaye anamaliza vipindi vyake viwili vya urais
Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa
wiki, Sitta alisema zaidi ya mambo hayo matatu, anaamini ana ushawishi
mkubwa na Watanzania wengi wanamwamini katika utendaji kazi wake.
“Nina mengi nimefanya kutokana na
historia yangu ya kiutendaji na ndiyo nitakayoitumia kama mtaji
utakaonibeba kwenye harakati hizi,” alisema.
Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa
Bunge la Katiba, alitaja mambo hayo matatu ambayo ni mtaji wake kuwa ni
uendeshaji wake wa chombo hicho cha kuandika Katiba, uendeshaji wake wa
Bunge na uzoefu wake wa muda mrefu kwenye nafasi mbalimbali alizowahi
kushika.
Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa
Bunge la Katiba, alitaja mambo hayo matatu ambayo ni mtaji wake kuwa ni
uendeshaji wake wa chombo hicho cha kuandika Katiba, uendeshaji wake wa
Bunge na uzoefu wake wa muda mrefu kwenye nafasi mbalimbali alizowahi
kushika.
“Niliendesha Bunge la Katiba kwa mafanikio na hata kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa,” alisema Sitta.
“Watanzania wataangalia wenyewe historia
yangu kwani mimi ndiye mwenyekiti niliyefanikisha kutimiza ndoto za
Watanzania kupata Katiba mpya kupitia Bunge Maalumu la Katiba, haikuwa
rahisi katika tukio hilo,” alisema.
Hata hivyo, Bunge la Katiba halikuisha
kwa maridhiano baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD kususia vikao kwa madai kuwa chombo hicho kiliweka
pembeni Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi.
Juhudi za Sitta kuwarejesha vikaoni ziligonga mwamba, lakini mchakato ukaendelea hadi Katiba Inayopendekezwa ilipopatikana.
Sitta alisema mtaji wake mwingine katika mbio za urais ni na kuimarisha demokrasia ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
“Mimi ndiye niliyebadilisha Bunge baada
ya kubadilisha kanuni za Bunge mwaka 2007, ambazo zilitoa uhuru, haki na
usawa kwa wabunge wote bila kujali wapinzani,” alijigamba.
NIPASHE
Mwanamke mmoja mkazi wa Mabibo mwisho,
Jijini Dar es slaam anadaiwa kuanzisha danguro la wasichana na kuendesha
biashara ya ngono ikiwamo ya jinsia moja.
Mwanamke huyo anayefahamika kwa jina la
mama Uzuri, anadaiwa kuwachukua wasichana hao kutoka vijijini kwa
kuwadanganya kuwa anakwenda kuwatafutia kazi mjini.
Inadaiwa kuwa fedha anazopata kutokana na biashara hiyo huzitumia kama gharama ya kuwatunza wasichana hao.
Wasichana hao kwa nyakati tofauti
walidai mwanamke huyo aliwachukua kijijini kwa lengo la akuwatafutia
ajira za ndani na wamesema wanaume wengi wamekuwa wakiwalazimisha
kufanya mepenzi bila kinga kwa madai kunawanyima starehe.
Walisema mwanzo walipoanza biashara hiyo walipata ugumu lakinikadri siku zilizvyokuwa zinakwenda waliizoea.
Gharama za biashara hiyo zinatofautiana
kutokana na kiwango cha mteja lakini kwa wale wanaofanyiwa tendo
kinyume na maumbile wateja hutozwa 20,000 na kawaida 5,000 hadi 10,000
kwa mara moja.
NIPASHE
Kitengo cha moyo hospitali ya Taifa
Muhimbili kinakabiliwa na upungufu wa madaktari 24 wa upasuaji hali
inayochangia upasuaji wa wagonjwa kushuka kutoka 16 hadi wawili kwa
siku.
Mkuu wa kitengo cha moyo Profesa Janabi
Mohamed alisema kuwa magonjwa ya moyo yanaongezeka kutokana na kukua kwa
uchumi hali inayosababisha wananchi kutofanya mazoezi, kula vyakula
vyenye mafuta yanayogeuka kuwa sumu na kushindwa kuchujwa na damu kuwa
nzito.
Alisema hali hiyo inasababisha mishipa kuwa mizito na matibabu yake ni upasuaji.
Alisema kitengo hicho kimeshafanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 453 tangu kianze miaka miwili iliyopita.
Alisema wagonjwa wengi wa moyo
wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma kunakochangiwa na umbali wa
kuwafikia wataalam wa moyo.
“Hapa tuna changamoto ya madaktari
bingwa wa upasuaji wa moyo kwa muda wa huu wako wane, kuna upungufu wa
madaktari 24, ambapo madaktari 12 ni wa kuzibua mishipa na wengine 12 ni
upasuaji wa moyo” Mohamed
No comments:
Post a Comment